Kuendelea mvutano wa kisiasa nchini Gabon
(last modified Tue, 06 Sep 2016 11:30:13 GMT )
Sep 06, 2016 11:30 UTC
  • Kuendelea mvutano wa kisiasa nchini Gabon

Mvutano wa kisiasa inaendelea kushuhudiwa nchini Gabon licha ya kupita siku kadhaa tangu kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais uliomrejesha tena madarakani Rais Ali Bongo.

Umoja wa Afrika kwa mara nyingine tena umesisitiza utayari wake wa kushiriki katika kutafuta njia za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa wa nchi hiyo. Katika taarifa yake ya hapo jana Umoja wa Afrika ulitangaza kuwa, uko tayari kuzisadia pande kuu zinazovutana nchini Gabon ili kuupatia ufumbuzi haraka mgogoro ulioibuka nchini humo baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa Rais.

Hii ni katika hali ambayo, machafuko na vurugu za baada ya uchaguzi zinashuhudiwa kuongezeka katika siku za hivi karibuni. Kushadidi hatua kali za kiusalama zimemfanya kiongozi wa upinzani anayedai kushinda katika uchaguzi huo awatake wapinzani wake wabakie majumbani na wasijitokeze katika mitaa na barabara za mji mkuu Libreville.

Jean Ping amekatakaa kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo na badala yake anasisitiza kwamba, yeye ndiye aliyeshinda kinyang'anyiro hicho, lakini akapokonywa ushindi. Kufuatia madai hayo ya Jean Ping Jumatano iliyopita mji mkuu Libreville ulishuhudia kuanza maandamano ya upinzani ya kupinga matokeo ya uchaguzi huo. Hali hiyo ilipelekea kutokea vurugu na mapigano kati ya waandamanaji na vikosi vya kutuliza fujo.

Machafuko ya Gabon

Kuendelea maandamano hayo kumepelekea pia kuongezeka idadi ya watu wanaotiwa mbaroni kila siku na vikosi vya usalama.

Huku anga ya Gabon ikikabiliwa na mvutano wa kisiasa, Saraphin Moundounga Waziri wa Sheria wa nchi hiyo amejiuzulu wadhifa wake kufuatia serikali kukataa kuhesabu upya kura za uchaguzi wa Rais uliosababisha ghasia na machafuko baada ya Ali Bongo kutangazwa mshindi kwa kumpita mpinzani wake Jean Ping kwa kura chache. 

Moundounga amesema kuhusu kujiuzulu kwake kuwa, ameamua kufanya hivyo kwa kuzingatia kuwa viongozi wa chama tawala nchini Gabon wameshindwa kutoa majibu yanayoridhisha kwa wasiwasi walionao wananchi kuwa, upo udharura wa nchi hiyo kuwa na amani na kwamba demokrasia inapasa kuimarishwa nchini humo.

Hata kama kabla ya hapo, wataalamu wa mambo walikuwa na wasiwasi juu ya yatakayotokea baada ya kutangazwa matokea ya uchaguzi wa Rais, lakini kuongezeka machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vya vyombo vya usalama dhidi ya raia kumeifanya hali ya mambo nchini humo kuwa mbaya zaidi.

Vitendo vya utumiaji mabavu vya vyombo vya usalama dhidi ya waandamanaji, kuongezeka kamatakamata ya kisiasa na kufungwa mitandao ya kijamii ni miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na serikali ambazo kwa hakika zimeongeza wasiwasi wa kushadidi anga ya hofu na woga katika nchi hiyo. Miaka kadhaa iliyopita pia, Gabon ilikumbwa na machafuko ya baada ya uchaguzi. 

Jean Ping, mgombea wa upinzani aliyeshindwa

Hivi sasa kwa mara nyingine tena wimbi la malalamiko na vitendo vya utumiaji mabavu limeigubika Gabon na kuifanya nchi hiyo itumbukie katika mgogoro. Jumuiya za kimataifa zimeendelea kuzitaka pande mbili hasimu nchini Gabon ziwe na subira na zifuatilie matakwa yao kwa njia zinazofaa.

Licha ya Gabon kuwa miongoni mwa nchi tajiri barani Afrika, lakini wataalamu wa mambo wanasema kuwa, kutokana na utajiri wa nchi hiyo kugawanywa kidhulma, hali hiyo imewafanya raia wa nchi hiyo kulalamikia sera za chama tawala.

Vyama vya upinzani vinakituhumu chama tawala kuwa kinajikusanyia utajiri  kwa madhara ya wananchi kwa kuingia mikataba ya muda mrefu na nchi za Magharibi hususan Ufaransa, na hivyo kuzipa fursa ya kupora madini ya nchi hiyo. Mazingira magumu ya kiuchumi, ukosefu wa ajira kwa vijana, umasikini wa raia na kutotekelezwa ahadi zilizotolewa na Rais Ali Bongo ni mambo ambayo yallipelekea wananchi wengi wanaotaka mabadailiko kumpigia kura mpinzani wa Rais Bongo yaani Jean Ping na hivi sasa hawakubaliani na matokeo yaliyomrejesha tena madarakani kiongozi huyo. Pamoja na hayo, inaonekana kuwa, anga ya kisiasa inayotawala nchini humo iko kwa namna ambayo hakuna upande kati ya pande mbili hasimu ambao uko tayari kuona kunakaririwa tena tajiriba chungu ya huko nyuma.

Filihali, kutangaza Umoja wa Afrika utayari wake wa kuwa mpatanishi wa mgogoro wa Gabon kwa upande mmoja na wito wa Jean Ping kwa wafuasi wake wa kukaa majumbani kwa upande mwingine ni mambo yanayoonesha juu ya kuweko juhudi za kuhitimisha mgogoro wa Gabon na kufuatiliwa matakwa kupitia njia nyingine.

 

Tags