Yahya Jammeh apinga matokeo ya uchaguzi wa Rais Gambia
Rais Yahya Jammeh wa Gambia ametangaza kuwa hatambui rasmi matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika nchini humo Disemba Mosi, ikiwa imepita karibu wiki moja tangu uchaguzi huo ufanyike na mgombea wa muungano wa upinzani kuibuka mshindi.
Yahya Jammeh ametangaza kuwa hatambui rasmi matokeo ya uchaguzi wa Rais uliofanyika Disemba Mosi mwaka huu ambapo alishindwa na mgombea wa muungano wa upinzani Adama Barrow. Yahya Jammeh ametaka ufanyike uchaguzi mwingine mpya wa rais. Jammeh ameyasema hayo ilhali siku kadhaa zilizopita yeye mwenyewe aliyakubali matokeo hayo ya uchaguzi wa Rais ambayo yangehitimisha utawala wake wa miaka 22 nchini Gambia.
Uchaguzi wa Rais nchini Gambia ulifanyika tarehe Mosi mwezi huu; ambapo mivutano ya kisiasa nchini humo ilipamba moto miezi kadhaa iliyopita. Vyama vya upinzani vilikubaliana kumsimamisha mgombea wa pamoja wa kuchuana na Rais Yahya Jammeh ili kuweza kuibuka na ushindi; hivyo hatimaye vilimuarifisha Adama Barrow kuwa mgombea wao wa kiti cha urais. Alieu Momarr Njai, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi ya Gambia alimtangaza Adama Barrow kuwa mshindi katika uchaguzi huo wa rais kwa kupata asilimia 45.5 ya kura.
Rais Yahya Jammeh alishika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 36.6 ya kura, na Mamma Kandie alishika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 17.8 ya kura. Tume ya Uchaguzi ya Gambia ilitangaza kuwa asilimia 65 ya wananchi walishiriki katika uchaguzi huo wa rais. Momarr Njai alimtangaza Adama Barrow mgombea wa muuungano wa vyama vya upinzani kuwa Rais halali kupitia taarifa iliyosomwa moja kwa moja katika televisheni rasmi ya Gambia. Hata kama wapinzani walifanya jitihada ili kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo, lakini misimamo iliyoonyeshwa na Yahya Jammeh kabla ya kufanyika uchaguzi na hatua zake za kiusalama kama vile kufunga mitandao ya kijamii na kuweka mipaka katika upatikanaji wa intaneti zilimpunguzia Barrow fursa ya kuibuka mshindi. Pamoja na hayo yote, hatimaye kile kilichowashangaza weledi wa mambo haikuwa kutangazwa mgombea wa muungano wa upinzani tu kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa rais, bali kukubali Rais Yahya Jammeh kuwa ameshindwa na kutamka kuwa atakabidhi madaraka. Kabla ya hapo, Rais wa Gambia alisisitiza katika kampeni za uchaguzi kuwa hatokubali matokeo yoyote yatakayoonyesha kuwa ameshindwa. Inaonekana kuwa moja ya sababu zilizomfanya Jammeh akubali matokeo ya uchaguzi huu wa rais ni nasaha na ushauri aliopata kutoka kwa washauri wake kwamba akubali kushindwa na pia kumshawishi akabidhi madaraka kidemokrasia.
Hata hivyo hivi sasa ikiwa imepita wiki moja tangu kufanyika uchaguzi huko Gambia na Rais Mteule akiwa tayari ametangaza mipango yake ya kazi, Yahya Jammeh jana alitangaza kupitia taarifa iliyosomwa na televisheni ya taifa kuwa, anapinga kikamilifu matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Gambia kwa namna kama ile ya awali ambapo alikubali kwa uaminifu matokeo ya uchaguzi huo, huku akiamini kuwa Tume Huru ya Uchaguzi ilikuwa yenye kuaminika, yenye kufuata ukweli na iliyo huru. Jammeh amesisitiza kuwa hatakubali matokeo ya uchaguzi wa rais na kwamba, uchaguzi mpya wa rais unapasa kufanyika kutokana na kilichotokea. Jammeh ameyazungumza hayo katika hali ambayo siku kadhaa zilizopita Rais Mteule Adama Barrow alieleza kufurahishwa na kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Gambia na kusisitiza juu ya ustawi wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake kulingana na matakwa ya wananchi. Barrow alibainisha kuwa atatumia nguvu ya kisiasa kutekeleza kwa usahihi uadilifu wa kijamii na mapatano ya kitaifa na kwamba, kuunda kamati ya uchunguzi ni moja ya hatua muhimu zilizo mbele yake. Rais Mteule wa Gambia aidha ametilia mkazo kufuatilia na kuchukua hatua kivitendo masuala kama kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa, kutekeleza kwa makini uadilifu katika sekta zote za serikali na kuwa na ustawi wenye malengo. Wananchi wa Gambia wanatarajia kushuhudia mivutano mikubwa mnamo siku zijazo kufuatia hali hii iliyojitokeza hivi sasa nchini kwao. Misimamo ya wapinzani na sisitizo lao la kuheshimiwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa, kutoridhishwa wananchi na hali waliyonayo na matarajio waliyonayo wakati wanasubiri kuanza duru mpya ya kisiasa nchini kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili, kunga'ng'ania Yahya Jammeh kubakia madarakani kupitia machafuko na ukandamizaji, yote hayo yanaweza kuzibadilisha siku zijazo huko Gambia kuwa za mchafukoge na mgogoro na kuanza mzozo wa kuwania madaraka na kupigania demokrasia nchini humo.