Mgogoro wa kisiasa nchini Niger
Asasi za kiraia nchini Niger zimetoa indhari juu ya uwezekano wa kuibuka mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Baada ya muungano wa upinzani kutangaza uamuzi wake wa kususia duru ya pili ya uchaguzi wa rais nchini Niger, Moussa Tchangari mmoja wa shakhsia mashuhuri wa jumuiya ya kiraia nchini humo amesema kuwa, nchi hiyo imeingia katika mgogoro wa kisiasa.
Moussa Tchangari ambaye anahesabiwa kuwa mmoja wa wapinzani wa rais wa sasa wa nchi hiyo Mahamadou Issoufou amesema kuwa, kususiwa duru ya pili ya uchaguzi wa rais na wapinzani ni hatua ambayo haina maslahi kwa nchi hiyo. Vyama vya upinzani nchini Niger vimeunda muungano unaojulikana kwa jina la COPA 2016. Viongozi wa muungano huo wametangaza kuwa, hautashiriki katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais iliyopangwa kufanyika Machi 20 kutokana na kutokuweko uadilifu katika mwenendo mzima wa uchaguzi huo. Vyama vya upinzani vinaamini kuwa, duru ya kwanza ya uchaguzi huo iliyofanyika tarehe 21 Februari ilitawaliwa na vitendo vya udanganyifu na wizi wa kura kwa maslahi ya mgombea wa chama tawala Rais Mahamadou Issoufou. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo jumla ya wagombea 15 walijitokeza kuwania kiti cha urais.
Kwa mujibu wa matokeo ya duru hiyo ya kwanza ya uchaguzi, Rais Mahamadou alipata asilimia 48 ya kura zote akifuatiwa na Hama Amadou aliyepata asilimia 18 na wawili hao kuingia katika duru ya pili.
Hama Amadou Waziri Mkuu wa zamani wa Niger alitiwa mbaroni katikati ya mwezi Novemba mwaka jana baada ya kurejea kutoka uhamishoni Ufaransa, akituhumiwa kuhusika katika magendo ya watoto wadogo na hadi sasa anaendelea kushikiliwa katika jela ya mji wa Filingué ulio umbali wa kilometa 180, kaskazini mwa mji mkuu Niamey. Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, tuhuma anazohusishwa nazo ni za kisiasa na kwamba, tangu awali serikali ya Rais Mahamadou Issoufou iliamua kumtia ndani ili kumzuia asiweze kushiriki katika uchaguzi wa mwaka huu.
Umoja wa Afrika ambao ulituma waangalizi 40 katika uchaguzi wa Niger umeonesha kuridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo licha ya kuweko kasoro za hapa na pale.
Uchaguzi wa Rais nchini Niger umeingia duru ya pili kutokana na kutopatikana mgombea aliyepata kura zilizopindukia asilimia hamsini. Mahakama ya Katiba nchini Niger nayo iliidhinisha duru ya kwanza ya uchaguzi huo lakini hakukutolewa taarigfa rasmi na mahakama kuhusiana na suala hilo.
Wapinzani nchini Niger wanaamini kuwa, kupunguzwa idadi ya vituo vya kupigia kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo ulikuwa ni ukiukaji wa Katiba. Viongozi wa muungano wa upinzani nchini Niger wanasema kuwa, rais wa sasa wa nchi hiyo na Mahakama ya Katiba ndio wanaobeba dhima ya hali ya sasa inayoikabili nchi hiyo.
Huku wapinzani wakisisitiza kususia uchaguzi huo, Baraza la Mawaziri la nchi hiyo limepasisha muswada unaotoa wito wa wananchi kushiriki katika uchaguzi huo na kwamba, kampeni za uchaguzi huo zitaanza tarehe 8 Machi.
Niger ni moja ya nchi masikini zaidi barani Afrika ambayo licha ya kuwa na vyanzo vingi vya utajiri wa madini ya urani, lakini bado ina hali mabaya ya kiuchumi. Vyovyote itakavyokuwa mwanasiasa yeyote atakayeibuka mshindi katika duru ya pili ya uchaguzi huo, atakuwa na kibarua kigumu cha kuivusha nchi hiyo katika hali yake mbaya ya hivi sasa kiuchumi.