Rais wa Nigeria aiita harakati ya Biafra katika meza ya mazungumzo
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35135-rais_wa_nigeria_aiita_harakati_ya_biafra_katika_meza_ya_mazungumzo
Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ameitaka harakati inayopigania kujitenga jimbo la Biafra la kusini mashariki mwa nchi hiyo kukaa katika meza moja ya mazungumzo na serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 02, 2017 10:45 UTC
  • Rais wa Nigeria aiita harakati ya Biafra katika meza ya mazungumzo

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria ameitaka harakati inayopigania kujitenga jimbo la Biafra la kusini mashariki mwa nchi hiyo kukaa katika meza moja ya mazungumzo na serikali.

Rais Buhari ametoa wito huo katika hadhara ya kikosi cha polisi katika mji wa Maiduguri wa kaskazini mashariki mwa nchi hiyo na kutangaza kwamba, serikali yake iko tayari kufanya mazungumzo na Harakati ya Biafra inayopigania kujitenga.

Rais wa Nigeria ametoa wito huo wa mazungumzo baada ya kuibuka mapigano kati ya vikosi vya usalama vya nchi hiyo na wafuasi wa Harakati ya Biafrika ya kusini mwa nchi hiyo inayopigania kujitenga.

Rais Muhamadu Buhari wa Nigeria

Rais Buhari sambamba na kulaani matakwa ya kujitenga nchini Nigeria amesisitiza kuwa, katu serikali yake haitaruhusu eneo fulani la nchi hiyo lijitenge na Nigeria na hivyo kufanikisha matakwa ya wanaopigania kujitenga.

Rais wa Nigeria sanjari na kuonya matokeo mabaya ya kujitenga amesema kuwa, serikali yake itakabiliana kwa nguvu zake zote na harakati ya aina yoyote ile inayotaka kujitenga eneo fulani la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Mbali na serikali ya Rais Buhari kukabiliwa na changamoto za harakati za kujitenga kama ya Biafra na Niger Delta, kwa sasa inakabiliwa na matatizo mengi likiwemo suala la kudorora uchumi na machafuko kufuatia harakati za kundi la kigaidi la Boko Haram hasa katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.