Msimamo wa Rais wa Nigeria kuhusiana na makundi yanayotaka kujitenga
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35149-msimamo_wa_rais_wa_nigeria_kuhusiana_na_makundi_yanayotaka_kujitenga
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesisitiza katika siku ya kuadhimisha uhuru wa nchi hiyo kuwa, hataruhusu nchi yake ianguke mikononi mwa wanaotaka kujitenga.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 03, 2017 00:30 UTC
  • Msimamo wa Rais wa Nigeria kuhusiana na makundi yanayotaka kujitenga

Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria amesisitiza katika siku ya kuadhimisha uhuru wa nchi hiyo kuwa, hataruhusu nchi yake ianguke mikononi mwa wanaotaka kujitenga.

Buhari aliyekuwa akitembelea eneo la kaskazi linalosumbuliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya wanachama wa kundi la Boko Haram ameliambia jeshi la nchi hiyo kuwa hataruhusu nchi ichukuliwe na wanaotaka kujitenga  na kusema: Jeshi la Nigeria litaendelea kuwa mstari wa mbele hadi pale Wanigeria watakapoweza kwenda kuishi kwa uhuru na amani katika eneo lolote ndani ya nchi hiyo. Kadhalika Buhari aligusia matatizo matatu yanayoikabili Nigeria kwa sasa ambayo ni ya kiusalama, kiuchumi na ufisadi na kusema kuwa, serikali yake inafanya juhudi za kuyatatua matatizo hayo.

Hatua ya Rais Muhammadu Buhari ya kuyatembelea maeneo hayo imekuja katika hali ambayo hivi sasa Nigeria inakabiliwa na matatizo na migogoro mingi.

Wapiganaji wa eneo la Biafra linalotaka kujitenga

Harakati za kundi la kigaidi na kiwahabi la Boko Haram hususan katika maeneo ya kaskazini mwa nchi zimepelekea kuongezeka machafuko na ukosefu wa usalama, kiasi kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa, hivi sasa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika ni moja kati ya nchi zinazokabiliwa na migogoro mikubwa ya kibinadamu duniani. William Lacy Swing, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhajiri ameonya kuhusu athari mbaya za mgogoro wa kibinadamu katika maeneo ya kaskazini mwa Nigeria. Japokuwa jeshi la Nigeria limekuwa likifanya jitihadi kubwa za kupambana na kundi hilo la kigaidi, lakini hadi sasa bado halijaweza kulitokomeza kikamilifu kundi hilo. Hii ni katika hali ambayo suala la kulitokomeza genge hilo hatari la kigaidi ilikuwa moja ya ahadi za Muhammadu Buhari katika kampeni za uchaguzi uliomuingiza madarakani nchini Nigeria.

Mgomo wa wafanyakazi kutokana na matatizo ya kiuchumi

Kuongezeka migogoro ya kikabila ni tatizo lingine ambalo limepamba moto zaidi katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni nchini humo na hivi sasa suala hilo limekuwa changamoto kubwa kwa serikali ya Abuja. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Nigeria inaundwa na jamii ya watu milioni 180 suala linaloifanya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika yenye idadi kubwa ya watu. Karibu makundi 250 tofauti ya kikabila yanaishi nchini humo. Hata hivyo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni migogoro ya kisiasa, mazingira mabaya ya kiuchumi, kukosekana usawa na ufisadi wa kupindukia kwa upande mmoja na pia uchochezi unaofanywa na pande za ndani na nje kwa ajili ya kuzusha tofauti za kikabila, kidini na kimadhehebu kwa upande wa pili, vimeyafanya baadhi ya majimbo ya nchi hiyo likiwemo jimbo la Biafra la kusini mashariki, kutaka kujitenga na serikali kuu ya Abuja.

Mashambulizi ya kundi la Boko Haram

Harakati za kutaka uhuru na kujitenga baadhi ya majimbo ya Nigeria inajiri katika hali ambayo siku chache zilizopita Rais Muhammadu Buhari alinukuliwa akisisitiza kuwa, suala la umoja wa kitaifa ni kadhia isiyo na mjadala. Ongezeko la matatizo ya uchumi ni kati ya matatizo makubwa ambayo yanaikabili Nigeria. Kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, kuongezeka gharama za kijeshi na kukosekana uwekezaji katika sekta za miundombinu na uzalishaji vinatajwa kuwa chanzo cha ongezeko la umasikini na ukosefu wa ajira nchini humo.

Mashambulizi ya kikabila

Ufisadi ni suala lingine ambalo licha ya serikali ya Rais Buhari wa Nigeria kusisitiza udharura wa kupambana nalo, lakini hadi sasa bado hajafanikiwa kulimaliza. Katika hali hiyo, Swaleh Habib Abdul-Raof mtaalamu wa masuala ya Nigeria anaamini kuwa, "Kukosekana idara thabiti, kutumiwa kisiasa kampeni za kupambana na ufisadi, kufanywa kwa usiri masuala ambayo yalitakiwa kuwekwa wazi na kadhalika utamaduni na itikadi potofu, ni mambo ambayo yamekwamisha mapambano dhidi ya ufisadi nchini Nigeria."

Katika mazingira hayo, sisitizo la Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria la kutaka kulindwa umoja wa kitaifa linaonyesha azma ya serikali ya Abuja ya kupambana na makundi yanayotaka kujitenga na kadhalika juhudi za kuboresha hali ya mambo nchini humo.