Watu 13 wauawa katika shambulio la kigaidi nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i35885-watu_13_wauawa_katika_shambulio_la_kigaidi_nchini_nigeria
Kwa akali watu 13 wameuawa nchini Nigeria kufuatia shambulio la kigaidi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 23, 2017 04:24 UTC
  • Watu 13 wauawa katika shambulio la kigaidi nchini Nigeria

Kwa akali watu 13 wameuawa nchini Nigeria kufuatia shambulio la kigaidi kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Vyombo vya usalama vya Nigeria vimetangaza kuwa, mtu aliyekuwa amejifunga mabomu alijiripua katikati ya kundi la watu katika mji wa Maiduguri ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria ambapo kwa uchache watu 13 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa. 

Majeruhi wa shambulio hilo la kigaidi wanaendelea kupata matibabu huku hali ya baadhi yao ikiripotiwa kuwa mbaya.

Licha ya kuwa hakuna mtu au kundi lililotangaza kuhusika na shambulio hilo la kigaidi lakini, vyombo vya usalama vya Nigeria vinaamini kuwa, aliyetekeleza shambulio hilo atakuwa mwanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Wanachama wa kundi la kigaidi la Boko Haram

Eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria linahesabiwa kuwa ngome ya kundi la kigaidi la Boko Haram ambapo harakati za kundi hilo katika maeneo hayo, zimehatarisha maisha na usalama wa wakazi wake ambao wengi wao wamelazimika kuyahama makazi yao.

Hivi karibuni watu wengine watano waliuawa baada ya gaidi mmoja kujiripua kwa bomu katika kijiji cha Belbelu, karibu na Kayamla, katika eneo la Konduga la jimbo lenye usalama mdogo la Borno, la kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 20,000 wameuliwa tangu mwaka 2009 katika hujuma na mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram na kuligeuza eneo la kaskazini mashariki mwa Nigeria kuwa moja ya sehemu zenye hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani kwa kuwafanya watu wasiopungua milioni 10 na laki saba wahitajie msaada ya kibinadamu.