Watu wenye silaha wauwa wanavijiji 10 nchini Nigeria
Watu waliokuwa na silaha wamewauwa watu kumi katika mashambulizi yaliyofanywa katika vijiji viwili vya wakazi wa jamii ya Kikristo katika jimbo la Kaduna huko kaskazini mwa Nigeria.
Maafisa wa jimbo hilo wamesema kuwa, watu sita waliuawa katika mkesha wa Sikukuu ya Krismasi wakati watu waliokuwa na silaha wanaoshukiwa kuwa wa kabila la Fulani walipolivamia eneo la Ungwan Mailafiya.
Mauaji hayo yalifuatia shambulio jingine katika eneo jirani la Nindem Ijumaa iliyopita ambapo watu waliokuwa na silaha waliufyatulia risasi mkusanyiko wa waumi mkutanoni na kuuwa watu wanne na kujeruhi kumi. Msemaji wa serikali ya jimbo la Kaduna amesema kuwa askari usalama wamepelekwa katika maeneo hayo ili kuzuia mashambulizi mengine.
Ni muda wa miongo mitatu sasa ambapo jimbo la Kaduna huko kaskazini mwa Nigeria limegubigwa na mauaji ya ulipizaji kisasi kati ya jamii asili za wakulima wa Kikristo na walowezi wa makabila ya Hausa na Fulani. Haki za kumiliki ardhi na malisho ya mifugo ndicho chanzo cha mzozo baina ya watu makabila hayo. Hata hivyo mzozo huo umegeuka na kuwa machafuko ya kikabila na kidini yalisababisha vifo vya mamia ya watu.