Kuendelea mashambulizi ya kigaidi nchini Nigeria; jimbo la Kaduna lashambuliwa
Polisi ya Nigeria imetangaza kuwa watu wawili wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea kaskazini mwa nchi hiyo.
Wanachama wa makundi ya kigaidi jana Jumatatu walikishambulia kijiji kimoja jimboni Kaduna katika siku ya kwanza ya mwaka mpya wa 2018 na kumuua kiongozi wa kijiji na mkewe.
Polisi ya Nigeria imeongeza kuwa, mtoto wa kiongozi wa eneo hilo pia amejeruhiwa na nyumba yake imechomwa moto.
Maafisa wa polisi wa Nigeria wameripoti kuwa hilo ni shambulio la tatu kufanywa na watu wenye silaha katika muda wa wiki moja katika jimbo la Kaduna. Wakati huo huo polisi ya Nigeria imetangaza kuwa idadi ya watu waliouawa katika shambulio la Jumamosi lililofanywa na kundi la kigaidi la Boko Haram dhidi ya wanavijiji katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria imefikia 25.
Hadi kufikia sasa watu zaidi ya elfu 20 wameuawa katika nchi za Nigeria, Cameroon, Niger na Chad na wengine zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuyahama makazi yao tangu kuanza mashambulizi ya kundi hilo la kigaidi mwaka 2009.