Waislamu wa Nigeria wataka Sheikh Zakzaky aachiwe huru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i38709-waislamu_wa_nigeria_wataka_sheikh_zakzaky_aachiwe_huru
Askari usalama wa Nigeria wamewashambulia watu aliokuwa wakifanya maandamano wakitaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo (IMN) na kumuuwa shahidi mfuasi mmoja wa kiongozi huyo wa kidini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 09, 2018 01:16 UTC
  • Waislamu wa Nigeria wataka Sheikh Zakzaky aachiwe huru

Askari usalama wa Nigeria wamewashambulia watu aliokuwa wakifanya maandamano wakitaka kuachiwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo (IMN) na kumuuwa shahidi mfuasi mmoja wa kiongozi huyo wa kidini.

Wafanya maandamano hao ambao waliandamana katika maeneo yasiyopungua 50 nchini Nigeria, wamemtaka Rais Muhammadu Buhari wa nchi hiyo atoe amri ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky. Maandamano hayo yamekabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa wanajeshi wa Nigeria ambao wamemuua shahidi muandamanaji mmoja katika jimbo la Kaduna.  

Maandamano hayo yamefanyika katika hali ambayo binti wa kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambaye yuko kizuizini amesema kuwa hali ya kimwili ya baba yake ni mbaya na kwamba serikali hairuhusu kiongozi huyo wa kidini apatiwe matibabu.

Nusaiba Zakzaky, binti ya Sheikh Ibrahim Zakzaky  
 

Kiharusi kilichompata hivi karibuni Sheikh Zakzaky akiwa kizuizini kimemzidishia hali mbaya ya kimwili kiasi kwamba, watu wa karibu na mwanazuoni huyo wamesema kuwa, upo uwezekano Sheikh Ibrahim Zakzaky akapata ulemavu mkubwa na kupooza viungo vya mwili na hata kushindwa kuzungumza.

Sheikh Zakzaky alipigwa risasi na wanajeshi wa Nigeria na kisha akatiwa nguvuni kufautia shambulio lililofanywa na jeshi la nchi hiyo mwezi Disemba mwaka 2015 katika Husseiniya ya mji wa Zaria. Karibu wafuasi elfu moja wa mwanazuoni huyo waliuliwa shahidi na mamia ya wengine kujeruhiwa katika shambulizi hilo. Yapata mwaka mmoja uliopita Mahakama Kuu ya Nigeria ilikutaja kutiwa nguvuni Sheikh Zakzaky kuwa ni kinyume cha sheria na kuamuru aachiwe huru haraka iwezekanavyo. Hata hivyo serikali ya Nigeria ingali inamshikilia Sheikh Zakzaky. 

Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa kizuizini na jeshi la Nigeria 

Ibrahim Suleiman mwanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ameashiria upinzani wa mara kwa mara wa serikali ya nchi hiyo dhidi ya ombi la harakati hiyo na familia ya Sheikh Zakzaky kwa ajili ya kumpeleka nje ya nchi kwa matibabu na akasema kuna uwezekano kwamba kunafanyika njama za kumuua shahidi taratibu Sheikh Zakzaky. 

Nigeria ni nchi yenye idadi kubwa ya Waislamu barani Afrika na ni miongoni mwa nchi tajiri na zenye maliasi ya mafuta. Nchi hiyo ambayo miaka ya nyuma ilikuwa ikidolewa jicho la tamaa na Marekani na waitifaki wake, hivi sasa inapewa mazingatio maalumu na baadhi ya nchi za Kiarabu ikiwemo Saudi Arabia ambayo inafanya jitihada za kujipenyeza na kueneza ushawishi wakee barani Afrika. Kwa msingi huo nchi hizo za Kiarabu hususan Saudia zinayausia silaha na kuyaunga mkono nyuma ya pazia baadhi ya makundi ya wanamgambo nchini Nigeria kwa shabaha ya kuzidisha mashinikizo kwa Waislamu hususan wale wa Kishia.

Waislamu hao pia wanakabiliwa na mashinikizo kutoka kwa viongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Katika siku kadhaa zilizopita baadhi ya wakuu wa kijeshi wa Nigeria walifanya mazungumzo na viongozi wa Israel na kuomba msaada wa kuimarisha jeshi na uchumi wa nchi hiyo. Uhusiano huo umekuwa sababu ya kuongezeka mashinikizo dhidi ya Waislamu wa Nigeria na kukabiliwa na vitendo vya mabavu na ukandamizaji. 

Yusuf Hamza mwanaharakati wa kisiasa wa nchini Nigeria ameashiria namna Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia zinavyohofia pakubwa  suala la kuenea zaidi madundisho ya Kiislamu kwa mujibu wa madhehebu ya wafuasi wa Ahlul Bait wa Mtume Muhammad (saw) huko Nigeria na kusisitiza kuwa: Kuna njama za wazi ya serikali ya Nigeria inayokusudia kumuuwa shahidi taratibu Sheikh Ibrahim Zakzaky kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.