Madaktari wasio na mipaka wasimamisha kazi zao kaskazini mwa Nigeria
Duru za kuaminika nchini Nigeria zimetangaza habari ya kusimamishwa kazi za madaktari wasio na mipaka kaskazini mwa nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram.
Televisheni ya al Jazeera imeripoti kuwa, shirika la madaktari wasio na mipaka wamesimamisha shughuli zao zote kaskazini mwa Nigeria baada ya genge la wakufurishaji la Boko Haram kuushambulia mji wa Rann katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Samantha Newport, msemaji wa shirika hilo amesema kuwa, wafanyakazi watatu wa kutoa misaada na askari wanane wa Nigeria wameuawa katika shambulio hilo la genge la Boko Haram.
Katika shambulizi jingine lililofanywa na genge hilo Alkhamisi usiku, mfanyakazi mmoja wa kutoa misaada alijeruhiwa na mwengine mmoja hajulikani alipo hadi hivi sasa.
Mashambulizi ya magaidi wa Boko Haram nchini Nigeria na katika nchi jirani za Chad, Niger, na Cameroon yameshapelekea zaidi ya watu 20 elfu kuuawa na milioni mbili na laki sita wengine kuwa wakimbizi.
Mwezi Januari mwaka huu, watu 12 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio la kujiripua kwa bomu lililofanywa sokoni katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Shambulio hilo lililofanywa mchana kweupe katika eneo la Muna Garage lenye kambi inayowahifadhi watu wasio na makazi nje ya makao makuu ya Maiduguri linadaiwa kufanywa na wanawake wanne waliokuwa wamejifunga mabomu.