Polisi: Watu 25 wameuawa katika mapigano mapya Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41647-polisi_watu_25_wameuawa_katika_mapigano_mapya_nigeria
Wafugaji wa kabila la Fulani wameua wanakijiji 25 katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria, kutokana na mzozo wa ardhi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 14, 2018 10:38 UTC
  • Polisi: Watu 25 wameuawa katika mapigano mapya Nigeria

Wafugaji wa kabila la Fulani wameua wanakijiji 25 katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria, kutokana na mzozo wa ardhi.

Kamishna wa Polisi katika eneo hilo, Undie Adie leo Jumatano ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, mauaji hayo yamefanyika katika eneo la Bassa, baada ya wanakijiji waliokuwa wakielekea katika kijiji cha Zirechi wakitokea eneo la Dundun kushambuliwa na wafugaji wa kabila la Fulani.

Amesema mbali na watu 25 kuuawa, wengine wawili wamejeruhiwa huku nyumba kadhaa katika kijiji cha Bassa zikiteketezwa kwa moto.

Gavana wa eneo hilo, Simon Lalong amewakosoa vikali watu wanaochochea mapigano hayo, na kufanya yachukue mkondo wa makabiliano ya kikabila, huku akisisitiza kuwa vyombo vya usalama vitakabiliana na wahalifu hao.

Wafugaji wa kabila la Fulani nchini Nigeria

Haya yanajiri siku chache baada ya watu 10 kuuawa katika mapigano baina ya wafugaji na wakulima katika kijiji cha Daffo, jimbo hilo la Plateau.

Mbali na hujuma hizo za kikabila, maeneo ya kati na kaskazini mashariki mwa Nigeria yamekuwa yakishuhudia mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na wanachama wa kundi la ukufurishaji la Boko Haram.