IMN: Serikali ya Nigeria itaendelea kumweka kizuizini Sheikh Zakzaky hadi afe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i41685-imn_serikali_ya_nigeria_itaendelea_kumweka_kizuizini_sheikh_zakzaky_hadi_afe
Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN) imesema serikali ya nchi hiyo inapanga kumweka kizuizini kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Zeenah hadi wafe.
(last modified 2026-03-03T12:46:59+00:00 )
Mar 15, 2018 04:22 UTC
  • IMN: Serikali ya Nigeria itaendelea kumweka kizuizini Sheikh Zakzaky hadi afe

Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria (IMN) imesema serikali ya nchi hiyo inapanga kumweka kizuizini kiongozi wa harakati hiyo Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe Zeenah hadi wafe.

Msemaji wa harakati hiyo S.I. Ahmad amehoji: "Je mataghuti wanaomshikilia shekhe shujaa wanasubiri muda ufike wamuue, kwa kuwa Allah alimuokoa na jaribio la kutaka kumuua kwa kutumia nguvu zao za kijeshi?"

Ahmad ameongeza kuwa Sheikh Ibrahim Zakzaky alipigwa risasi kwa karibu za kuweza hata kusababisha afe, lakini Mwenyezi Mungu alitaka abaki hai baada ya shambulio la kinyama na kikatili la mwezi Desemba. Amesema kiongozi huyo wa kidini amenyimwa kupatiwa huduma za tiba zinazostahiki pia lakini bado angali hai.

Msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria aliyasema hayo jana mwishoni mwa maandamano makubwa yaliyofanywa katika mji mkuu wa nchi hiyo Abuja kutoa wito kwa mara nyengine tena wa kuachiwa huru Sheikh Zakzaky.

Moja ya maandamano yaliyofanywa nchini Nigeria kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huruu

Mnamo tarehe 13 Januari na kufuatia uvumi kwamba Sheikh Zakzaky ameaga dunia kizuizini alikowekwa, kiongozi huyo wa kidini alionekana hadharani kwa mara ya kwanza tangu alipotiwa nguvuni Desemba mwaka 2015 na kushikiliwa kinyume cha sheria na vyombo vya usalama. 

Sheikh Zakzaky alipoteza uwezo wa kuona wa jicho lake la kushoto katika hujuma ya uvamizi uliofanywa na jeshi la Nigeria nyumbani kwake katika mji wa Zaria kaskazini mwa nchi hiyo.

Katika hujuma hiyo, mbali na yeye mwenyewe, mkewe pia alijeruhiwa vibaya, na zaidi ya wafuasi wake 300 wakiwemo wanawe watatu wa kiume waliuawa.

Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiwa huru Sheikh Zakzaky, serikali ya Abuja imekaidi amri hiyo na kuendelea kumweka kizuizini yeye na mkewe pamoja na idadi kubwa ya wafuasi wake kwa zaidi ya miaka miwili sasa.../