Nigeria katika mwaka wa nne tangu kutekwa nyara mabinti 200
Nigeria imeadhimisha mwaka wa nne tangu kutekwa nyara zaidi ya mabinti 200 wa shule ya sekondari huku ikikaririwa miito ili kuachiwa huru wanafunzi hao. Mabinti hao walitekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram lenye mfungamano na kundi la ukufurishaji la Daesh katika mji wa Chibok kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Shughuli ya kuwakumbuka wanafunzi hao ilianza jana Lagos mji mkubwa zaidi nchini Nigeria na zinaendelea hii leo huko Abuja mji mkuu wa nchi hiyo.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria kwa mara nyingine tena amewaahidi wazazi wa mabinti ambao wanaoendelea kushikiliwa na Boko Haram kuwa, kamwe mabinti hao hawawezi kusahauliwa au kutelekezwa licha ya kushikiliwa kwa muda mrefu.
Itakumbukwa kuwa jumla ya mabinti 219 walitekwa nyara na kundi la kigaidi la Boko Haram mwezi Aprili mwaka 2014 katika mji wa Chibok jimboni Borno.
Mabinti 112 kati ya 219 wanaendelea kushikiliwa na kundi hilo kwa muda wa miaka minne sasa. Aidha baadhi yao wamepatikana, wametoroka au kuachiwa huru kufuatia mwafaka uliofikiwa baina ya serikali na kundi hilo la kigaidi.