Kufikishwa mahakamani Sheikh Ibrahim Zakzaky na kufanyika kikao cha kimaonyesha
Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria (IMN) jana Jumanne alifikishwa mahakama kuu ya jimbo la Kaduna.
Sheikh Ibrahim Zakzaky ambaye ameendelea kushikiliwa kinyume cha sheria na vyombo vya usalama vya Nigeria alifikishwa mahakamani hapo pamoja na mkewe. Katika kikao cha jana Jumanne jaji kiongozi wa mahakama hiyo alimtaka Sheikh Zakzaky na mkewe kuwasilisha maombi rasmi ya maandishi ya kutaka kuachiwa huru kwa dhamana. Kesi hiyo imeakhirishwa hadi Juni 21, na wawili hao wamerejeshwa mjini Abuja.
Sheikh Ibrahim Zakzaky amefikishwa mahakamani ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama Kuu ya jimbo la Kaduna kutoa tuhuma mpya dhidi ya Sheikh Zakzaky kama vile kufanya mikutano kinyume cha sheria na kuvuruga utulivu, na kudai kuwa, wafuasi wa harakati hiyo walikuwa na silaha hatari.
Abdullahi Yola, msemaji wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria sambamba na kusema kuwa, madai hayo hayana msingi wowote ameeleza kuwa, tuhuma hizo zimetolewa katika fremu ya njama za serikkali za kuendelea kumshikilia kinyume cha sheria Sheikh Zakzaky, hasa kwa kutilia maanani kwamba, tuhuma hizo zimetolewa baada ya miaka miwili na nusu ya kushikiliwa kinyume cha sheria mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walijeruhiwa vibaya na kukamatwa katika shambulizi lililofanywa na jeshi la Nigeria tarehe 13 Disemba 2015 katika Husainia ya mji wa Zaria huko Kaduna, kaskazini mwa Nigeria. Mamia ya wafuasi wa harakati ya Kiislamu wakiwemo watoto watatu wa Sheikh Zakzaky waliuliwa shahidi katika uvamizi huo wa jeshi la Nigeria. Ijapokuwa baadaye, Mahakama Kuu ya Nigeria ilitoa amri ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky na mkewe, lakini hadi sasa jeshi na serikali ya nchi hiyo inaendelea kukaidi amri hiyo ya mahakama.
Kuendelea kushikiliwa kinyume cha sheria Sheikh Zakzaky kumewafanya Waislamu wa Nigeria waendelee kufanya mikusanyiko na maandamano kila mara wakitaka kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu. Hata hivyo hadi sasa serikali ya Nigeria si tu kwamba, imekataa katakata kuitikia wito huo, bali imezidisha mashinikizo dhidi ya Waislamu kwa kupiga marufuku mikusanyiko sambamba na kutumia mabavu kukabiliana na washiriki wa mikusanyiko na maandamano.
Miamala hiyo ya serikali na vyombo vya usalama vya nchi hiyo vimeifanya jamii ya Waislamu wa Nigeria iendelee kukabiliwa na mbinyo na mashinikizo. Kushadidisha mashinikizo, ukandamizaji dhidi ya Waislamu na kutoandaliwa mazingira mazuri kwa ajili ya maisha ya Waislamu hususan Mashia wa Nigeria ni sera zinazotekelezwa na serikali ya Abuja ambazo kimsingi zinafanyikka kwa ajili ya kukidhi malengo ya baadhi ya mirengo iliyo dhidi ya Waislamu.
Matukio ya kisiasa na kijamii nchini Nigeria yanaonyesha kuwa, Marekani, Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zina wasiwasi mkubwa na suala la kuongezeka ushawishi wa kimaanawi wa Waislamu hususan Mashia barani Afrika.
Hilo ndilo lililoyafanya madola hayo yaongeze himaya na uungaji mkono wao kwa serikali ya Nigeria ili iwashinikize zaidi Waislamju wa nchi hiyo hususan Waislamu wa madhehebu ya Shia katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Sheikh Adam Suhu, mjumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anasema kuhusiana na jambo hilo kwamba: Serikali ya Nigeria iko chini ya ushawishi wa siasa za Saudi Arabia, Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na madola yote hayo yamekuwa yakiendesha njama dhidi ya Waislamu hususan Mashia wa nchi hiyo.
Hivi sasa pia kufanyika kikao cha kimaonyesha cha kesi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky nako kumefanyika kwa lengo la kuongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu na kisingizio kingine kwa ajili ya kuendelea kumshikilia Sheikh Ibrahim Zakzaky.