UN yataka uchunguzi wa mauaji ya askari wa kulinda amani Mali ufanyike
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa mwito wa kufanyika uchunguzi wa mauaji ya askari wa Kikosi cha Kulinda Amani cha UN nchini Mali (MINUSMA), waliopoteza maisha baada ya gari lao kukanyaga bomu la kutegwa ardhini jana Ijumaa.
Amesema kuna haja ya kufanyika uchunguzi ili kubaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria haraka iwezekanavyo.
Askari wawili wa MINUSMA raia wa Sri Lanka jana Ijumaa waliuawa huku wengine sita wakijeruhiwa baada ya gari lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika mji wa Douentza, eneo la Mopti katikati ya nchi.
Kadhalika Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amelaani mauaji ya askari mwingine wa kikosi hicho cha UN nchini Mali, raia wa Burkina Faso aliyeuawa Alkhamisi ya juzi, baada ya kulengwa kwa bomu la kuelekezwa kutoka mbali.
Guterres amelaani kushtadi mauaji dhidi ya askari wa kulinda amani nchini Mali akisisitiza kuwa wahusika wataandamwa na mashitaka ya jinai za kivita kwa mujibu wa sheria za kimataifa.
Wiki iliyopita askari 10 wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA, waliuliwa na wengine wasiopungua 25 kujeruhiwa wakati wakijaribu kuzima shambulio la watu wenye silaha karibu na kijiji kimoja kaskazini mwa Mali.
Kikosi hicho cha MINUSMA na wanajeshi wa Ufaransa walitumwa nchini Mali mwaka 2013 kwa ajili ya kuwadhaminia usalama raia, lakini vikosi hivyo havijakuwa na utendaji wa kuridhisha katika kurejesha utulivu huku vitisho vya ugaidi vikiendelea kuitatiza nchi hiyo.