UN yachimbua makaburi 50 ya halaiki magharibi mwa Kongo DR
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51146-un_yachimbua_makaburi_50_ya_halaiki_magharibi_mwa_kongo_dr
Timu ya wataalamu wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) imefukua zaidi ya makaburi 50 ya umati magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kuripotiwa wimbi la mauaji yaliyotokea mwezi uliopita katika eneo hilo.
(last modified 2026-04-26T10:08:53+00:00 )
Jan 27, 2019 04:10 UTC
  • UN yachimbua makaburi 50 ya halaiki magharibi mwa Kongo DR

Timu ya wataalamu wa Ofisi ya Pamoja ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa (UNJHRO) imefukua zaidi ya makaburi 50 ya umati magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo baada ya kuripotiwa wimbi la mauaji yaliyotokea mwezi uliopita katika eneo hilo.

Mkurugenzi wa UNJHRO Abdoul Aziz Thioye, amesema, wamegundua zaidi ya makaburi 50 ya halaiki pamoja na mengine kadhaa ya mtu mmoja mmoja katika mji wa Yumbi ulioko magharibi mwa mkoa wa Mai-Ndombe.

Thioye ameongeza kuwa, kuna uwezekano idadi ya vifo ikawa kubwa zaidi kuliko inavyokadiriwa, kwa kuzingatia idadi ya maiti waliomo kwenye kila kaburi, kuanzia watano, kumi, mia moja au hata mia nne.

Jenerali Falla Sikabwe, mkuu wa jeshi magharibi mwa DRC ameviambia vyombo vya habari kuwa, uchunguzi wa pamoja wa timu ya kutafuta ukweli umeanza, ikijumuisha wataalamu wa Umoja wa Mataifa na maafisa wa eneo hilo.

Mapema mwezi huu, Umoja wa Mataifa ulisema, watu wasiopungua 890 waliuawa katika mauaji yaliyotokana na mapigano ya siku tatu kati ya jamii kadhaa za eneo hilo.

Michelle Bahelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa UN

Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alieleza kupitia taarifa aliyotoa tarehe 16 Januari kwamba, ofisi yake imetaarifiwa na "duru za kuaminika" kwamba kuna watu waliuawa katika vijiji vinne vya mji wa Yumbi kuanzia Desemba 16 hadi 18 mwaka jana.

Inavyoonekana, machafuko na mapigano, ambayo yanatokana na uhasama wa muda mrefu wa makabila mawili ya Banunu na Batende, yaliripuka baada ya watu wa kabila la Banunu kumzika chifu wao wa jadi katika eneo la ardhi ya kabila la Batende usiku wa Desemba 16.

Kwa mujibu wa ofisi ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa UN, katika machafuko hayo, nyumba na majengo yapatayo 465 yalichomwa moto au kuporwa, yakiwemo ya skuli mbili za msingi, kituo cha afya, soko na ofisi ya tume ya uchaguzi. 

Raia 16,000 pia walivihama vijiji hivyo na kukimbilia nchi jirani ya Jamhuri ya Kongo, inayojulikana pia kama Kongo-Brazzaville.../