Balozi wa Marekani 'apigwa bomu' katika maandamano nchini Malawi
Balozi wa Marekani nchini Malawi alikuwa baina ya wafuasi wa chama cha upinzani cha MCP ambao polisi ya Malawi imetumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatawanya kwa kushiriki kinyume cha sheria maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais uliofanyika Mei 21.
Hata hivyo msemaji wa Jeshi la Polisi la Malawi, James Kadadzera amesema askari polisi walifanya hivyo bila kujua kuwa balozi huyo wa Marekani nchini humo, Virginia Palmer alikuwa kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho cha upinzani.
Hii ni katika hali ambayo, Rais Peter Mutharika wa nchi hiyo ameutuhumu upinzani nchini humo kuwa unalenga kuipindua serikali yake.
Rais Mutharika amesema kuwa Lazarus Chakwera ambaye ni kiongozi mkuu wa upinzani na wafuasi wake wanapanga njama ya kuipindua serikali yake.
Upinzani nchini Malawi umekataa kuutambua ushindi wa Mutharika katika uchaguzi wa mwezi Mei. Kwa siku kadhaa sasa wapinzani wamekuwa wakiandamana wakidai kiongozi wao aliibiwa kura.

Chakwera ambaye alishindwa na Rais Mutharika kwa kura karibu 190,000 amesema hawezi kukubali na kumtambua mpinzani wake kama rais na ataendelea kushinikiza haki itendeke. Tayari amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Rais Mutharika.
Mutharika aliapishwa siku moja baada ya kutolewa matokeo ya urais yaliyokuwa yamecheleweshwa na Tume ya Uchaguzi ya nchi hiyo, lakini alitawazwa rasmi kuliongoza taifa hilo kwa muhula mwingine Mei 31 katika Uwanja wa Kitaifa wa Kamuzu katika eneo la Blantyre.