Marais wa nchi 10 za Afrika wauaga mwili wa Mugabe wa Zimbabwe
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i56003-marais_wa_nchi_10_za_afrika_wauaga_mwili_wa_mugabe_wa_zimbabwe
Marais wa nchi 10 za bara Afrika pamoja na marais wastaafu wameshiriki shughuli ya kuuaga mwili wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2019 11:44 UTC
  • Marais wa nchi 10 za Afrika wauaga mwili wa Mugabe wa Zimbabwe

Marais wa nchi 10 za bara Afrika pamoja na marais wastaafu wameshiriki shughuli ya kuuaga mwili wa Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Mwili huo umeagwa leo Jumamosi katika Uwanja wa Taifa mjini Harare. Miongoni mwa marais walioshiriki shughuli hiyo ni Uhuru Kenyatta wa Kenya, Edgar Lungu wa Zambia, Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Peter Mutharika wa Malawi na mwenyeji Rais Emmerson Mnangagwa.

Kadhalika Rais wa Singapore Halimah Jacon ameshiriki mazishi hayo. Kwa mujibu wa familia ya Mugabe, mwili wa kiongozi huyo utazikwa katika kipindi cha siku 30 zijazo, kinyume na taarifa za hapo awali kwamba ungelizikwa kesho Jumapili.

Familia ya Rais wa zamani wa Zimbabwe imekubali kiongozi huyo wa zamani azikwe kwenye makaburi ya mashujaa jijini Harare, hatua ambayo imemaliza mvutano uliokuwa unashuhudiwa kati ya serikali na familia ya Rais huyo wa zamani kuhusu wapi Mugabe aliyeongoza nchi hiyo kwa miaka 37 atazikwa.

Mugabe wakati wa uhai wake

Mugabe aliaga dunia Septemba 6 huko nchini Singapore alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mugabe ambaye aliiongoza Zimbabwe kwa karibu miongo minne tangu nchi hiyo ipate uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980 alilazimishwa kujiuzulu mwezi Novemba mwaka juzi baada ya mapinduzi ya jeshi.