Safaricom ya Kenya yapata leseni ya kuendesha shughuli nchini Ethiopia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i70432-safaricom_ya_kenya_yapata_leseni_ya_kuendesha_shughuli_nchini_ethiopia
Halmashauri ya Mawasiliano ya Ethiopia imelipatia shirika la Safaricom la Kenya leseni ya kutoa huduma za simu za mkononi nchini humo, hii ikiwa ni mara ya kwanza shirika lisilo la kiserikali kupewa leseni kama hiyo nchini Ethiopia.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 22, 2021 12:22 UTC
  • Safaricom ya Kenya yapata leseni ya kuendesha shughuli nchini Ethiopia

Halmashauri ya Mawasiliano ya Ethiopia imelipatia shirika la Safaricom la Kenya leseni ya kutoa huduma za simu za mkononi nchini humo, hii ikiwa ni mara ya kwanza shirika lisilo la kiserikali kupewa leseni kama hiyo nchini Ethiopia.

Safaricom itashirikiana na mashirika kadhaa yakiwemo ya Sumitomo la Japan na Vodacom, Vodafone na CDC ya Uingereza katika kutoa huduma hizo za simu za mkononi nchini Ethiopia.

Taariifa zinasema Safaricom imepata leseni hiyo baada ya kutoa kitita cha dola milioni 850 na hivyo kuipiku MTN ya Afrika Kusini ambayo ombi lake lilitupiliwa mbali baada ya kutoa pendekezo la dola milioni 600 tu.

Inakadiriwa kuwa ubia huo unaoongozwa na Safaricom utaweza kubuni nafasi za ajira zaidi ya milioni 1.5 nchini Ethiopia na kuwekeza kiasi cha dola bilioni 8.5 nchini humo katika kipindi cha miaka 10 ijayo.

Safaricom inatazamiwa pia kutuma satalaiti katika anga za juu ili kuimarisha huduma za intaneti kote nchini Ethiopia.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ametuma ujumbe katika Twitter na kusema uwekezaji huo wa Safaricom ndio mkubwa zaidi wa moja kwa moja wa kigeni katika historia ya Ethiopia.

Mashirika mengine ya kimataifa yaliyokuwa yanakodolea macho leseni iliyopewa Safaricom ni pamoja na Etisalat la UAE na Orange la Ufaransa.