Waislamu Burundi wamjia juu waziri aliyeivunjiwa heshima adhana
Waislamu Nchini Burundi wamemkosoa vikali waziri mmoja nchini humo kwa kuivunjia heshima Adhana, ambao ni mwito kwa Waislamu kwenda kutekeleza ibada ya Swala, moja ya nguzo muhimu za dini hiyo tukufu.
Kadhalika Waislamu hao wameendelea kupaza sauti za kutaka kuachiwa huru Sheikh Rashidi Ndikumana aliyekamatwa na polisi baada ya kumtaka Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi kuwaomba radhi Waislamu kufuatia tamko lake hivi karibuni la kuivunjia heshima Adhana.
Hii ni baada ya Waziri huyo aitwae Gervais Ndirakobuca kuongea kwenye mkutano na viongozi wa dini mbalimbali Burundi na kusema wananchi wanakerwa na kelele za Makanisa na Adhana za Misikiti.
Alidai kuwa, Adhana nyakati za alfajiri, ni kero kwa wananchi wa Burundi, na eti ni jukumu lao Waumini wa Kiislamu kujua wakati wa kusali bila kukumbushwa na Adhana.
Baada ya matamshi hayo kulizuka vuta nikuvute kati ya polisi na baadhi ya Waislamu katika mtaa wa Buterere kusini mwa Bujumbura ambako Sheikh huyo na Imama wa Masjid Madina anaishi.
Kiongozi huyo wa kidini Burundi alimtaka waziri huyo kutambua kwamba, Adhana katika Uislamu ilikuwepo hata kabla ya kuzaliwa kwake na itaendelea kuwepo; na akamuagiza kuwaomba radhi Waislamu katika kipindi kisichozidi wiki moja la sivyo watamuomba Rais Evariste Ndayishimiye wa nchi hiyo amfute kazi.