Raila aendelea kutafuta njia ya kujinasua kwenye mkwamo wa BBI
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i73846-raila_aendelea_kutafuta_njia_ya_kujinasua_kwenye_mkwamo_wa_bbi
Kiongozi wa Chama cha ODM nchini Kenya Bw Raila Odinga, natarajiwa kukutana na wabunge wote wa chama chake wiki hii, baada ya mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kugonga mwamba.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 23, 2021 08:51 UTC
  • Raila Odinga
    Raila Odinga

Kiongozi wa Chama cha ODM nchini Kenya Bw Raila Odinga, natarajiwa kukutana na wabunge wote wa chama chake wiki hii, baada ya mchakato wa kurekebisha Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) kugonga mwamba.

Mkutano huo pia utafanyika baada ya siasa za kutafuta miungano kabla uchaguzi wa mwaka wa 2022 kupata pigo kwa vile ilitarajiwa nafasi za uongozi katika serikali kuu zingepanuliwa kupitia kwa BBI.

Ijapokuwa ajenda ya mkutano huo haijatangazwa wazi, lakini Bw Raila Odinga anatarajiwa kutumia mkutano huo kupanga upya mikakati kuhusu uchaguzi ujao.

Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir amesema: “Ni wakati wa kuganga yajayo. Chama kitafanya mkutano wa wabunge wake wiki hii ambapo tutajadiliana kuhusu hatua tutakazochukua kuendelea mbele.”

Bw Odinga alitoa taarifa akisema chama cha ODM hakitaelekea katika Mahakama ya Juu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, lakini alidokeza kuwa suala la kutaka marekebisho ya katiba halijafika kikomo.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema, baadhi ya masuala yaliyopendekezwa katika BBI huenda yakapitishwa bungeni huku mengine yakifufuliwa baada ya 2022, hasa ikiwa waziri huyo mkuu wa zamani atafanikiwa kuunda serikali ijayo.

Miongoni mwa mapendekezo ya BBI ambayo huenda yakapitishwa katika Bunge la Kenya ni lile linalotaka mawaziri wawe wakichaguliwa kutoka miongoni mwa wabunge, na vilevile, magavana waruhusiwe kuchagua mawaziri wa kaunti kutoka miongoni mwa madiwani.

Siku chache zilizopita Mahakama ya Rufaa nchini Kenya, iliunga mkono uamuzi wa Mahakama Kuu, kuwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba nchini humo maarufu kama BBI, ni kinyume cha Katiba ya nchi hiyo na kutupilia mbali rufaa iliyowasilishwa kutaka maamuzi hayo yatenguliwe.

Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Majaji sita kati ya saba wa mahakama hiyo walimshtumu Rais Uhuru Kenyatta kuwa amekwenda kinyume cha Katiba kwa kuanzisha mchakato huo.

Mchakato wa kutaka kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo iliyopatikana mwaka 2010, ulianza baada ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, kumaliza uhasama wao kisiasa na kuungana ili kubadilisha mfumo wa uongozi nchini humo.