Miguna Miguna: Uchaguzi wa rais 2022 Kenya hautakuwa huru na wa haki
Wakili maarufu Mkenya, Miguna Miguna amedai kuwa uchaguzi wa urais wa 2022 hautakuwa wa kuaminika na kitakachofanyika ni kutawazwa kwa mgombea mmoja.
Miguna alisema Kenya haiwezi kuwa na uchaguzi wa haki, wa kuaminika, wa wazi na wa uwajibikaji wakati idara ya kitaifa ya kijasusi ndiyo itakayoamua mshindi.
Akizungumza katika kipindi cha kituo cha KTN, wakili huyo aliyehamishiwa nje ya nchi amedai kuwa hakutakuwa na uchaguzi mwaka ujao kwa vile tume ya uchaguzi si huru.
“Huwezi kufanya uchaguzi wakati tume ya uchaguzi haiko huru. Huwezi kuwa na uchaguzi wa haki, wa kuaminika, wa wazi na wa kuwajibika, wakati idara ya ujasusi ya kitaifa ndiyo inayoamua mshindi ni nani," amesisitiza Miguna.
Amegusia pia kuingiliwa kwa baraza la mawaziri, jambo ambalo amesema limependelea upande mmoja na litaweka hatarini mchakato mzima.
Wakili huyo mashuhuri Mkenya amekariri haja ya kufanyika marekebisho ya mfumo wa utawala wa Kenya na miundomsingi ya kuaminika ya uchaguzi ambayo inasimamiwa kwa mujibu wa sheria.
Amesema katika hali ya sasa, Kenya itakuwa na uchaguzi wenye utata na ametabiri migogoro nchini humo mwaka ujao.
Miguna Miguna aliyekuwa mgombea wa ugavana Kaunti ya Nairobi mnamo 2017 amesema ataanza safari ndefu ya kurejea Kenya Novemba 16 akiandamana na aliyekuwa jaji mkuu Willy Mutunga.
Miguna alikamatwa na Polisi Februari 2 mwaka 2018 kwa tuhuma za kushiriki kuapishwa kwa Raila Odinga kama Rais wa watu wa Kenya Januari, 30.
Baadaye mwanasheria huyo alifukuzwa Kenya na kupelekwa Canada.
Hatua hiyo ilipingwa na wanaharakati waliosema hakutendewa haki kwa sababu ni raia na mzaliwa wa Kenya.
Mbali na kuwa Mkenya, Miguna Miguna pia ana uraia wa nchi ya Canada.