Bomu la kutegwa ardhini laua watu 4 kaskazini mwa Kenya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i79946-bomu_la_kutegwa_ardhini_laua_watu_4_kaskazini_mwa_kenya
Watu wasiopungua wanne wamepoteza maisha baada ya gari lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika Kaunti ya Wajir, kaskazini mashariki mwa Kenya.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 03, 2022 09:21 UTC
  • Bomu la kutegwa ardhini laua watu 4 kaskazini mwa Kenya

Watu wasiopungua wanne wamepoteza maisha baada ya gari lililokuwa limewabeba kukanyaga bomu la kutegwa ardhini katika Kaunti ya Wajir, kaskazini mashariki mwa Kenya.

Duru za habari zinaarifu kuwa, watu wengine kadhaa wamejeruhiwa kwenye hujuma hiyo ya bomu ya jana Jumatano. Haijabainika iwapo gari lililohusika kwenye shambulio hilo ni la uchukuzi wa umma au la maafisa usalama.

Hili ni shambulio la pili la bomu kulenga gari katika eneo hilo la kaskazini mashariki mwa Kenya, mpakani na Somalia katika kipindi cha wiki moja iliyopita.

Jumatatu iliyopita, watu 10 walifariki dunia na wengine 13 kujeruhiwa katika shambulio la bomu lililolenga gari moja la abiria katika Kaunti ya Mandera kaskazini mwa Kenya.

Shambulio la bomu Mandera

Hakuna genge lililodai kuhusika na hujuma hizo mbili, lakini kundi la kigaidi la wanamgambo wa Al-Shabab limekuwa likiwalenga maafisa usalama na raia katika maeneo hayo ya kaskazini mashariki mwa Kenya katika mashambulio ya aina hiyo.

Wanachama wa kundi hilo la kigaidi wamekuwa wakitoa madai yasiyo na msingi kuwa wanaishambulia Kenya kwa kuwa nchi hiyo ya Afrika Mashariki imetuma wanajeshi wake Somalia.