Algeria: Ni makosa makubwa kuipa Israel hadhi na mwanachama mwangalizi AU
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i80044-algeria_ni_makosa_makubwa_kuipa_israel_hadhi_na_mwanachama_mwangalizi_au
Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa ni kosa makubwa sana kuupatia utawala haramu wa Israel hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika (AU).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 06, 2022 05:44 UTC
  • Ramtane Lamamra
    Ramtane Lamamra

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa ni kosa makubwa sana kuupatia utawala haramu wa Israel hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika (AU).

Ramtane Lamamra ameiambia televisheni ya France 24 akiwa Addis Ababa, kuwa hatua ya kuupa utawala wa Kizayuni wa Israel hadhi ya mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ilikuwa uamuzi mbaya wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, ambao ulichukuliwa bila ya kushauriana na wanachama wa umoja huo. 

Mgogoro wa kutambuliwa Israel kama mwanachama mwangalizi katika Umoja wa Afrika ulianza Julai mwaka jana wakati Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, alipoupatia utawala huo haramu hadhi ya kuwa mwanachama mwangalizi katika umoja huo na kusababisha mzozo mkubwa ndani ya chombo hicho.

Mapema jana Jumamosi Faki alitetea uamuzi wake, akidai kuwa unaweza kuwa "wenzo wa kuhudumia ya amani".

Harakati za ukombozi wa Palestina zimepinga madai hayo ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika huku Hamas ikitoa wito kwa Waafrika wote wanaopenda uhuru kupaza sauti ya mshikamano na taifa la Palestina na kumlazimisha Faki abatilishe uamuzi wake. 

Taarifa ya Hamas imeongeza kuwa: "Kutoa uanachama, japo hadhi ya kuwa mwangalizi tu kwa Israel, ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu pamoja na kanuni na sheria za AU, ambayo inapinga ubaguzi wa rangi na ukoloni.

Nchi nyingi za Kiafrika zinaitambua hatua ya Moussa Faki Mahamat ya  kuukubali utawala wa Kizayuni katika Umoja wa Afrika kama mwanachama mwangalizi kuwa ni kuyasaliti mapambano ya kupigania uhuru ya Palestina.

Algeria na nchi nyingine 13 wanachama wa Umoja wa Afrika zimetaka rasmi kufutwa uanachama wa utawala wa Kizayuni katika umoja huo na kulindwa thamani na nafasi ya Umoja wa Afrika.