Raila Odinga amtimulia kivumbi Ruto, kaunti ya Mombasa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i81614-raila_odinga_amtimulia_kivumbi_ruto_kaunti_ya_mombasa
Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ana kibarua kigumu kumpiku Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa umaarufu katika Kaunti ya Mombasa kabla uchaguzi ujao wa urais kwa mujibu wa matokeo ya utafiti.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 21, 2022 02:50 UTC
  • Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga
    Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga

Naibu Rais wa Kenya, William Ruto, ana kibarua kigumu kumpiku Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga kwa umaarufu katika Kaunti ya Mombasa kabla uchaguzi ujao wa urais kwa mujibu wa matokeo ya utafiti.

Uchunguzi uliofanywa na shirika la utafiti la Infotrak umebainisha kuwa, ushirikiano wa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, na Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, huenda ukamlemea sana Dkt Ruto katika eneo hilo.

Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa jana Jumapili yalibainisha kuwa, endapo Uchaguzi Mkuu ungefanywa leo, Bw Odinga angezoa asilimia 52 za kura Mombasa huku William Ruto akipata asilimia 29 pekee.

Kaunti ya Mombasa ndiyo huongoza kwa idadi ya wapigakura baina ya kaunti zote sita za Pwani na pia huaminika kutoa mwelekeo wa siasa za kitaifa katika ukanda huo.

Takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) zanaonyesha kuwa, katika mwaka wa 2017, kaunti hiyo ilikuwa na wapigakura 580,644.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka mwaka huu. Utafiti wa Infotrak pia umeonyesha kuwa, Bw Kalonzo Musyoka ambaye anaegemea upande wa Odinga, angepata asilimia moja tu za kura za urais, naye kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, aliye upande wa Dkt Ruto, angepata asilimia 0.1 za kura za urais Mombasa.

William Ruto

Hata hivyo, kuna asilimia 16 ya wapigakura ambao bado wanaweza kung’ang’aniwa na wanasiasa wanaomezea mate urais kwani idadi hiyo haijaamua yule wanayemtaka.

Kulingana na utafiti huo, Bw Odinga ana umaarufu wa zaidi ya asilimia 50 katika maeneobunge manne kati ya sita yaliyo Mombasa.

Kando na hayo, ripoti ya utafiti huo uliofadhiliwa na shirika la kutetea haki za binadamu la Haki Africa imeonyesha kwamba, Chama cha ODM kimedhibiti Mombasa kwa umaarufu.

Umaarufu wa ODM kaunti hiyo ni asilimia 46 huku kile cha United Democratic Alliance (UDA) ukiwa asilimia 24. Vilevile, umaarufu wa Muungano wa Azimio la Umoja ni asilimia 51 huku Kenya Kwanza ukiwa asilimia 23.