Mali yakataa wito wa UN kuhusu madai ya ukiukaji haki za binadamu
Serikali ya Mali imesema haitaufanyia kazi wito wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kuitaka iruhusu wanajeshi wa kulinda amani wasafiri ndani ya nchi hiyo kwa uhuru ili kuchunguza visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Balozi wa Mali kwenye Umoja wa Mataifa Issa Konfourou ameliambia baraza hilo kuwa, nchi yake haipo kwenye nafasi ya kuruhusu wanajeshi hao kuendelea na uchunguzi wao, bila ya ruhusa kutoka kwa serikali yake na kusisitiza kuwa serikali ya Bamako inawajibika kufanya uchunguzi huo.
Uamuzi huu wa Mali umekuja baada ya Baraza la Usalama la UN kuongeza muda wa kuhudumu kwa miezi mingine 12 vikosi vyake vya MINUSMA ambavyo vimekuwako katika taifa hilo la Afrika Magharibu kwa miaka tisa sasa.

Licha ya kupitishwa kwa azimio hilo la muda wa vikosi hivyo kuendelea kuwepo nchini Mali, Russia na China zilipiga kura ya hapana kupinga wanajeshi hao kuchunguza madai ya uwepo wa visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
Katika ripoti yake, vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA vimesema, vimerekodi visa 320 vya ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanyika nchini humo kati ya mwezi Januari na Machi mwaka huu.../