Kongamano la kubainisha fikra za Imam Hussein AS lafanyika Kenya
Kongamano la kubainisha Harakati ya Imam Hussein AS, Imamu wa Tatu wa Mashia limefanyika katika mji wa Mombasa nchini Kenya na kuhudhuriwa na wasomi wa Kiislamu kutoka pembe zote za nchi hiyo na pia nchi jirani.
Kwa mujibu wa taarifa, kongamano hilo ambalo ni la tano la kuangazia pande tofauti za harakati ya Imam Hussein AS, limeandaliwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Al Qaim ikishirikiana na Bilal Muslim Mission na wadau wengine wakati wa kukaribia Mwezi wa Muharram.
Kongamano la Imam Hussein AS linalenga kuarifisha utamaduni wa Imamu huyo kwa Waislamu wa Kenya na jamii nzima ya nchi hiyo.
Wasomi mbali mbali wa Kiislamu wakiwemo wahuburi na wanaharakati wamehutubu katika kongamano hilo ikiwa ni katika mkakati wa kujitayarisha kuupokea Mwezi wa Muharram.
Katika mwezi wa Muharram Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki kote duniani hukumbuka tukio la Ashura ambalo lilijiri takribani miaka 1383 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria.
Katika tukio hilo, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura.
Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.
Wimbi la mwamko wa Imam Hussein AS dhidi ya madhalimu lilikuwa na taathira kubwa mno na ambayo haikuishia kwenye wakati, zama au eneo makhsusi bali imeendelea kufanya kazi yake kati ya wanadamu wote hadi katika zama hizi. Ukweli huu umethibitisha msemo unaosema: "Kila siku ni Ashura na kila ardhi ni Karbala."