World Vision International: Njaa inaendelea kuongezeka miongoni mwa watoto Kenya
Shirika lisilo la kiserikali la misaada ya kibinadamu la World Vision International limetahadharisha kuhusu ongezeko la njaa na vifo miongoni mwa watoto nchini Kenya.
Watoto katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya ambayo yanakabiliwa na ukame hula makaroni zilizorutubishwa kwa siagi na karanga, ambazo ni aina ya chakula tiba. Uzalishaji na upatikanaji wa makaroni zilizorutubishwa umekuwa mgumu zaidi sasa tangu kuanza vita huko Ukraine.
James Jarso kutoka shirika la Word Vision anasema: Kutashuhudiwa vifo vingi iwapo vyakula hivi vya thamani vilivyo na kalori nyingi, vitamini na madini muhimu vitapungua. Ameongeza kuwa, katika hali ambayo watoto milioni 1.7 katika eneo la Pembe ya Afrika wanakabiliwa na hatari ya njaa; bei ya bidhaa za chakula ikiwemo makaroni yaliyorutubishwa na mengineyo imeongezeka tangu kuanza vita nchini Ukraine.
Amesema, chakula hiki cha ajabu kinaweza kuleta kinaweza kuokoa maisha ya mtoto katika hali ngumu huko Marsabit, ambapo wafanyakazi wa misaada wanasema, watoto wadogo wanaangamia katika mazingira yanayokaribiana na njaa.
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) pia ambao unanunua karibu asilimia 80 ya makaroni ya aina hiyo umetiwa wasiwasi na suala hilo.
Ukraine ni muuzaji mkubwa wa mafuta ya alizeti, ngano na nafaka nyinginezo duniani, na vita vinavyoendelea nchini hiyo vimeathiri bei na upatikanaji wa bidhaa mbalimbali duniani. Shirika la UNICEF limetabiri kuwa, bei za bidhaa hizo zitaongezeka kwa asilimia 16 hadi kufikia mwezi Novemba mwaka huu ikilinganishwa na kabla ya kuanza vita huko Ukraine.
Bei za bidhaa zinapanda katika kipindi kibaya zaidi ambapo watoto zaidi ya milioni 1.7 walio na umri chini ya miaka mitano wanataabika kwa utapiamlo mkali huko Kenya, Ethiopia na Somalia.