Dawa zilizopitwa na wakati kutoka Ulaya zahangaisha Waafrika
Asilimia 42 ya dawa zilizopigwa marufuku katika masoko ya bara Ulaya tangu mwaka 2012, zinauzwa katika nchi za bara Afrika.
Hayo yamebainishwa na Dakta Gaoussou Fadiga, tabibu na mtafiti mashuhuri kutoka Guinea ambaye ameongeza kuwa, kumekuweko na ongezeko la watu wanaougua ugonjwa wa figo barani Afrika kutokana na matumizi ya dawa ambazo muda wake wa matumizi umepita.
Kwa mujibu wa utafiti wa Dakta Gaoussou Fadiga, mamilioni ya wagonjwa wa figo wanaendelea kuteseka kutokana na dawa hizo zilizotoka bara Ulaya.
Utafiti wa Maktaba ya Taifa ya Dawa ya Marekani umeonyesha kuwa, ugonjwa sugu wa figo (chronic kidney disease) katika nchi za bara Afrika ni mara tatu au nne zaidi kuliko nchi zilizostawi kiuchumi.
Dakta Fadiga amesema ushirikiano kati ya serikali za Afrika, Shirika la Afya Duniani WHO na taasisi za kimatibabu ndio njia pekee ya kukata mishipa ya kusafirishwa dawa zilizopitwa na wakati kutoka bara Ulaya hadi katika masoko ya nchi za Afrika.