Marubani wa Shirika la Ndege la Kenya Airways kuanza mgomo kesho Jumamosi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i90052-marubani_wa_shirika_la_ndege_la_kenya_airways_kuanza_mgomo_kesho_jumamosi
Marubani wa Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, wanatarajiwa kuanza mgomo kesho kutilia mkazo madai yao ya mazingira bora ya kazi, licha ya mahakama ya nchi hiyo kuamuru mgomo huo usitishwe.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 04, 2022 07:52 UTC
  • Marubani wa Shirika la Ndege la Kenya Airways kuanza mgomo kesho Jumamosi

Marubani wa Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways, wanatarajiwa kuanza mgomo kesho kutilia mkazo madai yao ya mazingira bora ya kazi, licha ya mahakama ya nchi hiyo kuamuru mgomo huo usitishwe.

Tangazo hilo la mgomo limetolewa na maafisa wa muungano wa wafanyakazi hao. Hatua hiyo inajiri siku moja baada ya notisi ya mgomo wa wiki mbili kutolewa na muungano wa marubani ambao wanalitaka shirika hilo kurejesha michango kwa hazina yao ya kustaafu.

Katika taarifa yake leo, Chama cha Marubani wa Mashirika ya Ndege ya Kenya (KALPA) kimesema kuwa, wanachama wao hawataripoti kazini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kuanzia kesho Jumamosi saa kumi na mbili asubuhi kwa saa za Kenya. Notisi ya mgomo wa siku 14 ya chama hicho ilimalizika Jumatano, lakini shughuli katika shirika la ndege zilibaki bila kukatizwa hadi Alkhamisi.

 Kenya Airways inayomilikiwa na serikali ya Kenya ni mojawapo ya mashirika makubwa ya usafiri wa anga barani Afrika, ikiunganisha miji mingi katika mabara ya Afrika, Asia na Ulaya na hivyo mgomo huo utasababisha adha na usumbufu mkubwa kwa wasafiri wengi.

 

Katibu Mkuu wa chama cha marubani wa Kenya Airlines, Kapteni Murithi Nyaga, amesema hakuna ndege ya shirika hilo itakayopaa kutoka Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta mjini Nairobi kuanzia saa 12 asubuhi kesho Jumamosi. Amesema, uongozi wa shirika hilo umeshindwa kushughulikia malalamiko ya marubani. Siku ya Jumatano Shirika la Ndege la Kenya, Kenya Airways lilionya kwamba malalamiko ya marubani hao hayana uzito wa kuhalalisha mgomo.

Mapema wiki hii, Kenya Airways ilitangaza kuwa, haiwezi kurejesha michango kwa hazina ya ruzuku ya marubani hadi mwakani 2023.