UN yataka kufanyike uchunguzi kuhusu mauaji kaskazini mwa Burkina Faso
Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kufanyika uchunguzi haraka iwezekanavyo kuhusu madai ya kuuliwa raia kaskazini mwa Burkina Faso.
Seif Magango amesema kuwa, kuna udharura wa kufanyika uchuanguzi haraka iwezekanavyo kuhusu madai kwamba jeshi la taifa limeuwa raia kaskazini mwa nchi hiyo. Magango ameongeza kuwa, serikali ya Burkina Faso Jumamosi iliyopita ilitoa taarifa ikieleza kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma hizo.
Vikosi vya ulinzi na usalama vya Burkina Faso (FDS) na vile vya kujitoea kwa ajili ya ulinzi wa nchi hiyo (VDP) vinatuhumiwa kuuwa raia wengi katika vijiji kadhaa karibu na eneo la Djibo kaskazini mwa nchi hiyo. Msemaji wa Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, wanawake na watoto ni miongoni mwa raia hao wa Burkina Faso wanaodaiwa kuuliwa na jeshi na kwamba kuna tuhuma zenye mashiko kuhusu jinai hizo.
Wakati huo huo, vyombo kadhaa vya habari vimetangaza kuuliwa karibu raia 50 katika mashambulizi ya tarehe 9 mwezi huu wa Novemba. Hii si mara ya kwanza ambapo jeshi la Burkina Faso (FDS) na kikosi cha kujitolea cha wanamgambo (VDP) kinatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya raia wa nchi hiyo.