Homa ya Dengue yaua makumi ya watu nchini Sudan
Mamlaka za afya nchini Sudan zimetangaza habari ya kuaga dunia makumi ya watu kutokana na mripuko wa homa ya Dengi (Dengue) nchini humo.
Montasir Mohamed Osman, Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Majanga na Dharura katika Wizara ya Afya ya Sudan amesema watu 26 wameaga dunia katika majimbo tisa ya nchi hiyo kufikia sasa.
Osman ameeleza kuwa, kesi 462 za maradhi hayo zimethibitishwa katika mripuko wa sasa, huku nyingine 3,439 zikishukiwa kuwa za homa hiyo.
Afisa huyo wa Wizara ya Afya ya Sudan amesema akthari ya kesi hizo zimerekodiwa katika majimbo ya Kordofan Kaskazini, Kordofan Magharibi na Darfur Kaskazini.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, kesi zaidi ya 1,060 za homa ya Dengue zimenakiliwa nchini Sudan katika mripuko wa sasa ulioanza mwezi uliopita wa Oktoba.

Homa ya Dengeu ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambapo ueneaji wake unafanana na ule wa malaria. Huambukizwa na virusi vya mbu aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoadoa meupe yenye kung'aa.
Dalili za ugonjwa huo huanza kujitokeza siku tatu mpaka 14 baada ya mtu kuambukizwa. Mtu mwenye homa ya Dengi huwa na dalili za homa ya ghafla, kuumwa kichwa, uchovu wa mwili, maumivu ya maungo na misuli, kichefuchefu na kutapika, kuwashwa macho, muwasho na kuwa na vipele vidogo vodogo.