Jeshi la Mali 'lawasamehe' askari 49 wa Ivory Coast
Kiongozi wa kijeshi nchini Mali ametangaza habari ya kuwapa msamaha makumi ya wanajeshi wa Ivory Coast waliokamatwa nchini humo mwezi Julai mwaka uliomalizika 2022, wakituhumiwa kuwa mamluki.
Kanali Abdoulaye Maiga, msemaji wa serikali ya Mali alisema hayo jana Ijumaa katika taarifa na kuongeza kuwa, "Msamaha uliotangazwa na Rais wa Mali, Kanali Assimi Goita kwa mara nyingine unaonesha kujitolea kwake kwa masuala ya amani, mazungumzo, uanamajimui wa Afrika, na kulinda uhusiano na ushirikiano na nchi za eneo."
Taarifa hiyo ingawaje haijaeleza ni lini askari hao wataondoka gerezani lakini imeeleza kuwa, uamuzi huo 'huru' unaashiria kujitolea kwa Rais wa Mali katika masuala ya uongozi bora na kuimarisha uhusiano na nchi jirani haswa Ivory Coast.
Haya yanajiri wiki moja baada ya mahakama moja huko Bamako, mji mkuu wa Mali kuwahukumu kifungo cha miaka 20 jela wanajeshi 46 wa Ivory Coast baada ya kuwapata na hatia ya 'kuhujumu' usalama wa taifa hilo jirani yake. Askari watatu wanawake miongoni mwao waliachiwa huru mwezi Septemba mwaka 2022, lakini walikuwa wamehukumiwa kunyongwa bila ya wao kuwepo mahakamani.
Mali na Ivory Coast zilitumbukia katika mzozo wa kidiplomasia tangu Julai 10 mwaka uliomalizika wa 2022, baada ya maafisa wa Mali kuwatia nguvuni wanajeshi 49 wa Ivory Coast mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bamako.
Serikali ya Mali inayoongozwa na wanajeshi ilisema kuwa, wanajeshi hao wa Ivory Coast hawakuwa na nyaraka zozote za kuarifisha ujio wao huko Mali na kwamba iliwatambua kama mamluki. Wanajeshi hao walituhumiwa kujaribu kuvuruga usalama wa Mali na kisha wakaweka korokoroni.
Serikali ya Ivory Coast kwa upande wake ilisema kuwa wanajeshi hao walikwenda Mali kwa ajili ya shughuli za kawaida za kuunga mkono kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani nchini Mali. Kodivaa hapo awali iliishutumu Mali kwa kuidai fidia na kuamiliana na wanajeshi wake hao 46 kama wahalifu baada ya kutiwa nguvuni na serikali ya Bamako.