Pezeshkian: Iran ipo tayari kuimarisha uhusiano na Ivory Coast
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imejiandaa kikamilifu kupanua ushirikiano wa pande mbili na Ivory Coast ili kufikia malengo ya pamoja.
Wakati wa hafla ya kupokea hati za utambulisho za balozi mpya wa Ivory Coast mjini Tehran, Tamakolo Ouattara jana Jumanne, Rais Pezeshkian alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano na nchi za Kiafrika kama kipaumbele muhimu katika sera ya kigeni ya Iran.
Pezeshkian ameeleza matumaini kwamba, balozi mpya atafanya kazi kwa bidii kufikia malengo haya wakati wa misheni yake hapa nchini.
Rais wa Iran ameangazia kuanzishwa kwa tume ya pamoja ya kiuchumi kama hatua muhimu katika kuunda sera na mifumo ya ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.
Rais amesisitiza tena kwamba Iran, katika juhudi zake za kupanua uhusiano na nchi zote, inasisitiza mara kwa mara kuwepo kanuni za maadili, uhusiano wa kibinadamu, amani, utulivu na usalama wa kimataifa.
Ameeleza matumaini yake kuwa, kuwepo kwa balozi huyo nchini Iran kutafungua njia ya kuimarisha uhusiano wa kirafiki na kupanua ushirikiano wa pamoja katika nyanja mbalimbali.
Kwa upande wake, balozi huyo amewasilisha salamu kutoka kwa Rais wa Ivory Coast, Alassane Ouattara kwa Rais Pezeshkian na kusisitiza kwamba, diplomasia inapaswa kutumikia masilahi ya pande zote na kuimarisha urafiki kati ya mataifa. Ameeleza azma yake kubwa ya kutimiza azma hiyo muhimu nchini Iran.
Balozi Ouattara pia amekiri nafasi kubwa ya Iran katika uhusiano wa kikanda na kimataifa na uwezo mkubwa ndani ya nchi. Amesisitiza nia ya Ivory Coast ya kuendeleza ushirikiano na Iran katika nyuga zote.