Ujumbe wa Kiongozi Muadhamu Mpya wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137344-ujumbe_wa_kiongozi_muadhamu_mpya_wa_iran
Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe wake wa kwanza kulihutubia taifa la Iran.
(last modified 2026-03-13T16:14:16+00:00 )
Mar 13, 2026 16:14 UTC
  • Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei
    Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei

Ayatullah Sayyid Mojtaba Husseini Khamenei, Kiongozi mpya wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe wake wa kwanza kulihutubia taifa la Iran.

Baada ya kuanza kwa Jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu na kumswalia Mtume wake Mtukufu Muhammad (saw) pamoja na kizazi chake kitoharifu, hasa Imam wa Zama, Imam Mahdi (f), Ayatullah Mojtaba Khamenei ametoa salamu zake za dhati za rambirambi kutokana na watu waliouawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Marekani na utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran, hasa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Ali Khamanei (MA).

Amewaombea dua ya heri watu wa Iran, bali Waislamu wote duniani waliojitolea kwa dhati kwa ajili ya kuhudumia Uislamu, zikiwemo familia za mashahidi wa mwamko na Muqawama wa Kiislamu, hasa wale wote waliopoteza maisha yao katika hujuma ya hivi karibuni ya maadui wa Uislamu, ikiwemo familia yake yeye mwenyewe, Ayatullah Mojtaba Khamenei.

Katika sehemu ya pili ya ujumbe wake, mbali na kulishukuru taifa shupavu la Iran ya Kiislamu, amezungumzia uamuzi wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Iran na kusema, yeye mwenyewe hakuwa na habari kwamba alikuwa amechaguliwa kuliongoza taifa hili, bali alipata habari hiyo kupitia matangazo ya televisheni ya taifa, kama walivyofanya Wairani wengine. Amesema pamoja na kukubali uamuzi huo lakini litakuwa jambo gumu kwake kujaza pengo lililoachwa na viongozi wawili wakuu waliomtangulia, yaani Imam Ruhullah Khomeini na baba yake, Ayatullah Ali Khamenei (MA).

Ayatullah Mojtaba Khamenei amesema itakuwa vigumu sana kujaza pengo lilioachwa na shakhasia kama baba yake, Ayatullah Ali Khamenei ambaye amekuwa katika medani ya Jihadi na kuhudumia nchi kwa miaka 60, na kujiepusha na aina zote za anasa na starehe, ambapo aligeuka kuwa lulu inayong’ara na sura ya kipekee, sio katika zama zetu hizi tu bali pia katika historia yote ya viongozi wa nchi hii. Amesema: Maisha yake na namna alivyouawa shahidi vinaashiria utukufu na heshima iliyotokana na kumtegemea Mwenyezi Mungu pamoja na kupigania haki na uadilifu duniani. Amesisitiza kwamba itachukua muda mrefu kwa watu wengi kupata kumjua kwa undani na kiuhalisia. Amesema mtu anapozingatia masuala haya ndipo ugumu wa kujaza pengo lililoachwa na mtu kama huyo unapodhihiri zaidi. Pamoja na hayo amesema anatarajia kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu mazito yaliyo mbele yake, kwa kutegemea msaada wa Mwenyezi Mungu na uungaji mkono wa watu wa Iran.

Ayatullah Mojtaba Khamenei amesisitiza kuwa nafasi ya wananchi katika uendeshaji wa masuala ya nchi ina umuhimu mkubwa na kwamba hilo lilionekana wazi katika kipindi ambacho hakuwepo Kiongozi Mkuu wa zamani na kutojazwa nafasi hiyo kwa siku kadhaa. Amesema wananchi walisimamia mambo vizuri, bila kushuhudiwa tatizo lolote na uongozi mkuu nchini.

Amesema ili kufanikiwa zaidi katika uwanja huo watu wote wanapasa kumtegemea kwa dhati Mwenyezi Mungu na kutawasali kwa nuru za Maasumina watukufu (as), jambo ambalo linawadhaminia kila aina ya ushindi na mafanikio dhidi ya maadui. Amesema hii ndiyo siri na sifa kubwa ya ushindi wao, ambayo maadui wao hawana. Amewataka wananchi waendelee kulinda umoja na mshikamano wao wa kitaifa ambao hadi sasa umewawezesha pakubwa katika kuvuka mitihani na changamoto mbalimbali. Ayatullah Khamenei amewaomba wananchi wa Iran wawazingatie Waislamu wenzao katika pembe tofauti za dunia kupitia muqawama na mapambano yao na kusaidiana wao kwa wao nyakati za matatizo na changamoto. Amezitaka taasisi zote nchini kufanya kila liwezekanalo kwa ajili ya kuwahudumia kwa dhati wananchi wanaojitolea na kujituma kwa ajili ya kulinda nchi na dini yao tukufu ya Uislamu.

Akizungumzia hasara iliyosababishwa na maadui nchini kutokana na mashambulizi yao ya kichokozi, Ayatullah Khamanei amesema kwamba, bila shaka Jamhuri ya Kiislamu itamtaka adui afidie hasara iliyopatikana, na kwamba ikiwa atakataa kufanya hivyo, Iran itafidia hasara hiyo kwa kutwaa mali za adui kwa kiasi kinachohitajika, la sivyo itafanya uharibifu wa kiwango cha hasara iliyosababishwa na adui katika mali zake.

Katika nukta ya tano ya ujumbe wake, Ayatullah Mojtaba Khamenei amewahutubu viongozi wa baadhi ya nchi za eneo la Magharibi mwa Asia. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikifuatilia kuwa na uhusiano na ujirani mwema na nchi zote 15 zilizo na mpaka wa pamoja wa nchi kavu na majini na Iran, kwa manufaa ya mataifa yote husika.

Pamoja na hayo amesikitika kuona kwamba baadhi ya nchi hizo zimekuwa zikiweka vituo vya kijeshi na kifedha vya nchi za Magharibi na zilizo na uadui na Uislamu katika ardhi zao kwa ajili ya kuziwezesha kudhibiti eneo hili nyeti la Asia Magharibi. Amesikitika kwamba vituo hivyo vimetumika katika mashambulizi yanayoendelea hivi sasa dhidi ya Iran. Amesema: Katika kujibu mashambulizi ya adui, Iran imekuwa ikivilenga vituo hivyo tu, na sio maslahi ya nchi jirani. Amesema nchi hizo zinapaswa kuweka wazi misimamo yao kuhusu wale wanaoshambulia taifa la Iran na watoto wake wadogo wakiwa shuleni. Amezitaka nchi hizo kufunga vituo hivyo, kwa sababu wenyewe wamethibitisha kivitendo kuwa madai ya Marekani kuwa itawadhaminia usalama ni hadaa na uongo mtupu. Amesema hilo litawadhania usalama wa kweli, kuimarisha uhusiano wao na Iran na kuwaepusha na udhalilishaji wanaofanyiwa na nchi za Magharibi zinazomiliki vituo hivyo.

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Ayatullah Mojtaba Khamenei amemuenzi tena Kiongozi Shahidi mwendazake, ambaye amesema ameacha jeraha na huzuni kubwa katika nyoyo za watu wengi nchini na duniani. Amesema Kiongozi Shahidi alitamani sana kufa shahidi na kwamba amejibiwa dua yake hiyo ya muda mrefu katika mwezi mtukufu wa Ramadhani. Amesema alipitia machungu mengi kwa heshima, nguvu na uvumilivu bila moyo wake kuwa na dhiki.

Amemhakikishia Kiongozi Shaidi kuwa atafanya kila awezalo na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuendelea kupeperusha bendera ya mapambano na Muqawama dhidi ya maadui wa Uislamu, na kutetea maslahi na malengo matukufu ya taifa la Iran, kama alivyofanya yeye mwenyewe mwendazake wakati wa uhai wake.

Amemalizia kwa kutoa shukrani zake za dhati kwa viongozi na watu wote waliomuunga mkono, kumpongeza na kumshajiisha kuhudumu katika nafasi yake mpya ya Kiongozi Mkuu wa mfumo wa Kiislamu wa Iran.