Mfumo Mpya wa Dunia
Je, hadi sasa umewahi kufikiria mfumo huu unaotawala dunia ulitoka wapi?
Msingi wa Dunia Mpya urarudi nyuma kwenye matukio ya Ulaya katika karne za 15 na 16. Kufuatia maendeleo ya sayansi jarabati na mafanikio ya teknolojia, wazo liliibuka taratibu kwamba, dunia ya jadi na ya kizamani pamoja na sehemu zake nyingi, kama vile falsafa, dini na maadili, vinapaswa kuwekwa kando.
Wazo lolote ambalo lilikuwa nje ya ulimwengu wa kimaada na unaohisika na kuonekana, lilipuuzwa na kutengwa.
Katika mazingira hayo, kukusanya mali nyingi kupindukia, madaraka na anasa vilikuwa lengo kuu la watu binafsi na serikali. Matokeo ya mtazamo huu yalikuwa ushindani mkali kati ya mataifa ya Ulaya kwa ajili ya kupanua eneo lao la utawala na kupata rasilimali zaidi.
Wakati huo huo, fikra ya "ubora wa mbari ya watu Ulaya" au wazungu ilifanywa kisingizio cha madola ya kikoloni kunyakua sehemu kubwa za dunia na kupora rasilimali na nguvukazi za mataifa mbalimbali.
Kwa mfano, kufikia mwanzoni mwa karne ya 20, ufalme wa Uingereza ulidhibiti karibu robo ya idadi ya watu duniani na karibu robo ya eneo la nchi kavu ya sayari ya dunia.
Mashindano hayo hatimaye yalisababisha vita viwili vya dunia vilivyokuwa na uharibifu mkubwa. Yaliibua Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia ambavyo vilikuwa na taathira kubwa katika historia ya mfumo wa ulimwengu.
Baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia mnamo 1945, muundo mpya ulianza kudhihiri: Kuasisiwa Umoja wa Mataifa, kuundwa taasisi za kiuchumi kama vile Mfuko wa Fedha wa Kimataifa na Benki ya Dunia, na kuanza ushindani kati ya mataifa mawili makuu, yaani Marekani na Umoja wa Kisovieti.
Katika kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu uliingia kivitendo katika mfumo wa kambi mbili, ambapo nchi nyingi zililazimika kuegemea upande mmoja wa kambi hizo za Mashariki na Magharibi, ili kuendelea kubakia hai na kuishi.
Kufuatia kusambaratika Muungano wa Kisovieti mwaka 1991, wengi walidhani kwamba ulimwengu ulikuwa umeingia katika hali ya kambi moja tu yenye nguvu ikiongozwa na Marekani.
Lakini historia haijawahi kusimama. Leo, nguvu mpya zinaendelea kudhihiri.
Sasa, huku kukiwa na migogoro ya kijiopolitiki na vita vipya — hasa mapigano ya sasa ambayo yanaihusisha Iran na moja ya nguvu kuu duniani —, swali la msingi linaulizwa tena:
Je, mfumo wa zamani wa dunia unasambaratika? Na je, mfumo mpya wa dunia utakuwaje na utaendeshwa na nani?