Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu waanza mjini Tehran
-
Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, Tehran
Mkutano wa 40 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu umeanza mjini Tehran, ukijikita zaidi kwenye maono ya Kiongozi marehemu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Shahidi Sayyid Ali Khamenei kuhusu kuimarisha umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu.
Mkutano huo umefunguliwa leo Alhamisi katika hafla iliyohudhuriwa na Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, na mamia ya wasomi na wanafikra Waislamu kutoka takriban nchi 40 duniani.
Karibu wageni 600 wa ndani na nje ya nchi wakiwemo watu mashuhuri katika taaluma mbalimbali, utamaduni na dini kutoka nchi za Kiislamu kama vile Iraq, Pakistan, Uturuki, Lebanon, Afghanistan, na nchi za Ghuba ya Uajemi, pamoja na mabalozi kadhaa walioko Tehran wamehudhuria hafla ya ufunguzi.
Mkutano wa Tehran unafanyika chini ya kaulimbiu "Umoja wa Kiislamu katika Mtazamo wa Imam Shahidi, Ayatullah Sayyid Ali Hosseini Khamenei."
Mkutano wa 40 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulioanza leo Tehran umelenga kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu, kukuza ushirikiano baina ya wasomi na wanafikra wa kidini, na kusaidia kuunganisha mitazamo ya kisayansi na kitamaduni katika Umma wa Kiislamu.
Katika ujumbe wake kwa mkutano huo, mwanazuoni wa ngazi ya juu wa Iran, Ayatullah Hussein Noori Hamedani amesema kuwa umoja wa Waislamu umekuwa muhimu katika historia yote ya Uislamu, lakini umuhimu wake ni mkubwa zaidi hii leo kwa kuwa maadui wa Uislamu wanajaribu kuwadhoofisha wafuasi wa diini hiyo, kupanda mbegu za hitilafu na migawanyiko na kuzidhibiti nchi za Waislamu.
" Suala hili limepata umuhimu mkubwa zaidi kwa sasa, wakati maadui wa Uislamu wanapotumia uwezo wao wote kudhoofisha Waislamu, kuzua migawanyiko na kuzitawala nchi za Kiislamu," amesema Ayatullah Noori Hamedani na kuongeza kuwa "udharura wa kimantiki na wajibu wa kidini" wa umoja unadhahirika zaidi hivi sasa kuliko wakati wowote ule.
Amesema Qur'ani Tukufu inawataka Waislamu kushikamana ibarabara na kamba ya Mwenyezi Mungu, na inakataza waziwazi hitilafu na migawanyiko inayopelekea kudhoofika na kupotea kwa nguvu na utukufu wao.
Ayatullah Noori Hamedeani amesisitiza kuwa wanazuoni wa Kiislamu wana jukumu kubwa katika suala hili na wanapaswa kuzuia hitilafu za kidini zisitumiwe vibaya na maadui wa Uislamu.
"Marekani na Israel zimekuwa mstari wa mbele miongoni mwa wale wanaotaka kuzidhoofisha nchi za Kiislamu," amesisitiza Ayatullah Hamedani.