Pezeshkian: Marekani haitapata chochote kupitia mashinikizo ya kiuchumi dhidi ya Iran
-
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa Marekani haitaweza kufanikisha lolote kupitia mashinikizo ya kiuchumi, akisisitiza kuwa Iran itaendelea kusimama imara.
Pezeshkian amebainisha haya katika mkutano uliofanyika Benki Kuu ya Iran jana Jumatano ambapo alipitia viashiria vya hivi karibuni vya masuala ya fedha, sarafu za kigeni na uchumi akiwa pamoja na Waziri wa Uchumi Ali Madanizadeh, Gavana wa Benki Kuu Abdolnaser Hemmati, na kundi la wachumi mashuhuri wa Vyuo Vikuu.
Mkutano huo umefanyika katika mazingira ambayo Rais Pezshkian ameyataja kuwa ya kipekee, yaliyotokana na vita, mzingiro wa kiuchumi na mashinikizo kutoka nje. Mkutano huo umefanyika baada ya tangazo la kampeni ya Marekani ya kuiwekea Iran mashinikizo ya kiuchumi.
Rais Pezeshkian ameeleza kuwa sekta za uchumi za serikali zimeandaa hatua za kukabiliana na mashinikizo hayo, huku akisisitiza kuwa Marekani haitaweza kufikia malengo yake kupitia mashinikizo ya kiuchumi.
"Kama ambavyo Marekani haikuweza kufanikisha lolote wakati wa vita—licha ya ushujaa wa vikosi vya jeshi pamoja na msaada na uungaji mkono wa wananchi; vivyo hivyo haitaweza kufanikisha lolote kupitia mashinikizo ya kiuchumi katika hatua hii pia," amebainisha Rais wa Iran katika mkutano uliofanyika Benki Kuu jana Jumatano.
Pezeshkian aliongeza kuwa msimamo wa serikali ni kufikia maelewano na kutatua masuala kupitia ushirikiano na mazungumzo, huku ikidumisha msimamo thabiti dhidi ya mashinikizo ya kiuchumi.
Wakati huo huo Rais wa Iran amezishukuru taasisi za serikali na sekta binafsi ambazo, licha ya matatizo na changamoto zote, zimeendeleza juhudi zao katika "jihadi ya kiuchumi," zikikidhi mahitaji ya maisha ya wananchi na kudumisha utulivu wa soko.