Mar 02, 2023 11:48 UTC
  • Mapigano ya waasi wa M23 na jeshi la Congo yaendelea kaskazini magharibi mwa Goma

Mapigano baina ya kundi la waasi wa M23 na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaripotiwa kuendelea magharibi mwa Goma na kuzidi kuzusha wasiwasi miongoni mwa wananchi.

Ripoti zaidi zinasema kuwa, mapigano hayo yamepelekea baadhi ya raia wa maeneo hayo kuyakkimbia makazi yao.  Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema kuwa,  Mkuu wa ujumbe wa kulinda amani huko DRC (MONUSCO), Bintou Keita kwa sasa yuko mashariki mwa nchi hiyo.

Jana mkuu huyo wa MONUSCO alikutana na Gavana wa kijeshi wa jimbo la Ituri  ambaye aliomba msaada wa tume ya kulinda amani kuendelea kujenga uwezo wa vikosi vya usalama vya Congo.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, uchunguzi uliofanywa na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ulibaini hivi karibuni kuwa wanachama wa kundi la waasi la M23 waliwaua wanaume wasiopungua ishirini na kuwabaka wanawake na wasichana wengi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

 

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikiituhumu jirani yake mdogo Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yamekanushwa na Rwanda, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.

Ripoti iliyotolewa hivi karibuni na wataalamu huru wa Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa, jeshi la Rwanda lilihusika kwenye "operesheni za kijeshi" dhidi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika maeneo yanayokabiliwa na machafuko mashariki mwa DRC.