May 16, 2024 07:25 UTC
  • UK, Ufaransa na Ujerumani zaonywa kwa kutuma ndege kuilinda Israel katika Operesheni ya Ahadi ya Kweli

Brigedia Jenerali Esmail Qa’ani, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ametoa onyo kwa Uingereza, Ujerumani na Ufaransa baada ya nchi hizo tatu za Troika ya Ulaya kupeleka ndege zao za kivita kuulinda utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya operesheni ya kulipiza kisasi ya Ahadi ya Kweli iliyofanywa na Iran mwezi uliopita wa Aprili.

Qa'ani amesema, wahalifu wote wanapaswa wajue kwamba hatua na uhalifu wao umebaki kwenye mafaili ya matendo yao.

Akifafanua zaidi, Kamanada Mkuu wa Kikosi cha Quds cha IRGC amesema: "Ufaransa, Ujerumani, na Uingereza zisifikirie kuwa zilipeleka ndege tu usiku ule na kwamba suala lile lilikuwa limekwisha. Ni sawa, usiku ule ulipita, lakini zitawajibishwa katika wakati mwafaka”.

Kwa mujibu wa Qa’ani, Marekani na muungano mzima wa kijeshi wa Magharibi wa NATO ulichangia uwezo wao wote wa kijeshi katika kuulinda utawala ghasibu wa Kizayuni dhidi ya operesheni ya Iran.

Amefafanua zaidi kwa kusema: "makundi saba hadi manane ya manowari yalitumwa Bahari Nyeusi kuzuia operesheni" na akaongeza kuwa zaidi ya ndege 200 pia zilisambazwa katika anga ya eneo wakati wa usiku wa operesheni hiyo.

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshili la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa ushindi wa operesheni ya Ahadi ya Kweli hautokani na idadi ya makombora tu na ndege zisizo na rubani ambazo zilifika maeneo yaliyokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni bali kuna siri nyingi zilizojificha ndani ya operesheni hiyo ambazo zitachukua muda mrefu kuzihakiki na  kuzichambua.

Aidha, amezishauri nchi za eneo hili na nje ya ukanda huu zijifunze kutokana na kushindwa Marekani kuulinda utawala haramu wa Israel wakati wa operesheni ya Iran, na kuzitaka nazo pia zisijifariji sana kwa kuitegemea Washington.

Jenerali Qa'ani aliyasema hayo jana alipohutubia hafla iliyofanyika kwa mnasaba wa kuadhimisha Arubaini ya kuuawa shahidi Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi, kamanda wa Kikosi cha Quds cha IRGC.

Brigedia Jenerali Zahedi, na maafisa watano aliokuwa pamoja nao waliuawa shahidi Aprili Mosi katika shambulio la kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran katika mji mkuu wa Syria, Damascus.

Katika kulipiza kisasi, mnamo Aprili 13, IRGC iliyalenga na kuyapiga maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa msururu wa ndege zisizo na rubani na makombora. Mashambulizi hayo ya kulipiza kisasi yaliyopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli yalisababisha uharibifu mkubwa kwa vituo vya kijeshi vya Israel katika maeneo hayo.../

 

Tags