Mafanikio ya uvumbuzi wa wanawake wa Iran katika nyanja mbalimbali
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111838-mafanikio_ya_uvumbuzi_wa_wanawake_wa_iran_katika_nyanja_mbalimbali
Ingawa bado kuna pengo kubwa kati ya wavumbuzi wanawake na wanaume duniani lakini viashiria vilivyopo vinaonyesha kuwa juhudi zinazofanywa na wanawake wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuziba pengo hilo zinaendelea kwa kasi kubwa.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
May 17, 2024 03:39 UTC
  • Mafanikio ya uvumbuzi wa wanawake wa Iran katika nyanja mbalimbali

Ingawa bado kuna pengo kubwa kati ya wavumbuzi wanawake na wanaume duniani lakini viashiria vilivyopo vinaonyesha kuwa juhudi zinazofanywa na wanawake wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuziba pengo hilo zinaendelea kwa kasi kubwa.

Kwa kauli ya Mitra Aminluo, Mkurugenzi wa Kituo cha Usimamizi wa Vipawa vya Kifikra na kwa mujibu wa utafiti alioufanywa na Kitengo cha Masuala ya Kielimu kuhusu uvumbuzi uliosajiliwa nchi Iran,katika miaka mitano iliyopita, ushiriki wa wanawake katika usajili wa uvumbuzi umeongezeka kwa asilimia tano 5. Idadi hii ilikuwa karibu asilimia 26 mwaka 2022 ambayo ni  asilimia 10  zaidi ya wastani wa kimataifa.

Idadi ya wavumbuzi wanawake wa Iran ni kubwa kuliko wastani wa ulimwengu 

Takwimu hizi mwaka wa kabla yake yaani 2021 zilikuwa asilimia 24 ambayo ilionyesha ongezeko la karibu asilimia mbili kwa mwaka, na hii ni katika hali ambayo kwa wastani wa dunia, asilimia ya wavumbuzi wanawake katika mafaili ya uvumbuzi ni asilimia 14 na hata katika nchi zilizoendelea kiwango hicho huwa hakifikii asilimia 18. Kwa maneno mengine ni kwamba nchini Iran kati ya kila wavumbuzi wanne wanaume, kuna mwanamke mmoja mvumbuzi, ambapo kimataifa idadi hiyo ni wavunvuzi 6 wanaume kwa kila mwanamke.

Miundombinu na fursa ambazo zimetolewa kwa wanawake na wasichana wa Kiirani kushiriki katika nyanja mbalimbali za kielimu nchini baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hatua kwa hatua zimewaandalia mazingira mazuri ya kufanikiwa katika nyanja tofauti za uvumbuzi na ubunifu.

Hivi sasa zaidi ya asilimia 50 ya wanachuo, asilimia 40 ya wafanyakazi, asilimia 33 ya wanachama wa majopo ya kielimu katika vyuo vikuu na karibu asilimia 50 ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini Iran inaundwa na wanawake. Vile vile baada ya Mapinduzi ya Kiislamu waandishi zaidi ya 9,500 na wachapishaji 840 ni wanawake wanaojishughulisha na msuala mbalimbali katika nyanja hizo nchini Iran.

Kwa mujibu wa ripoti ya Forbes, kufuatia ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuongezeka uadui wa madola makubwa dhidi ya nchi hii, Tehran ilichukua hatua ya kuufanya mfumo wa elimu nchini kuwa wa bure usiokuwa na malipo ili kuongeza uwezo wake wa kushindana katika nyanja mbalimbali na kukidhi mahitaji ya nchi, ambayo yamekuwa yakiwekewa vikwazo mbalimbali na maadui.

Jambo hili limepelekea kuanzishwa vyuo vikuu vingi vya serikali katika miji na vijiji katika pembe zote za nchi na kufanya elimu ya ngazi ya juu ipatikane kirahisi zaidi kwa wanawake na wasichana wa Iran, suala ambalo hatimaye limeimarisha mchango wa wanawake katika maendeleo ya nchi.

Mafanikio na maendeleo makubwa ya wanawake baada ya Mapinduzi ya Kiislamu

Bila shaka, maendeleo ya jamii yoyote ile yanategemea uwezeshaji na ushirikishwaji wa watu wote katika jamii hiyo, na ni wazi kuwa kuwezeshwa wanawake katika nyanja mbalimbali katika jamii ya Kiislamu sio tu kwamba ni njia muhimu ya kupata maendeleo endelevu, bali kwenyewe ndio lengo la maendeleo.

Kwa kuzingatia kwamba moja ya viashiria na makadirio ya kutathmini maendeleo na ustawi wa uvumbuzi katika kila nchi ni kiwango cha kusajiliwa uvumbuzi, hivyo mchango wa wanawake kuhusu suala hilo, ni moja ya viashiria muhimu vya kutathmini uwiano wa kijinsia katika uwanja huo. Licha ya makelele na propaganda nyingi zinazopigwa na nchi za Magharibi kuhusu kutetea haki za wanawake, lakini mchango na nafasi ya wanawake katika nyanja za kielimu, hususan katika uwanja wa uvumbuzi sio kubwa hivyo.

Mwishoni mwa karne ya 20 ni asilimia 10 tu ya nadharia zote zilizosajiliwa zilihusishwa na wanawake ambapo kwa sasa ni chini ya asilimia 30 ya watafiti wote duniani inaundwa na wanawake. Suala hili lilipelekea Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutangaza Februari 11 kuwa "Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana kuhusu Elimu" kwa lengo la kuongeza ushiriki wao na kuwawezesha katika uwanja huo.

Pamoja na hayo utafiti wa Ofisi ya Uvumbuzi ya Nchi za Ulaya (EPO) unaonyesha kwamba pengo kubwa lililopo kati ya wavumbuzi wanaume na wanawake kuhusu masuala ya kielimu barani humo halitaweza kuzibwa kabla ya mwaka 2070.

Katika upande wa pili, miundombinu ya kielimu na kisayansi iliyoandaliwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya wanawake na wasichana nchini imejenga matumaini kwamba mchakato wa kuongezeka mchango wa wanawake wa Iran katika uvumbuzi wa kielimu utaendelea kupanuka  na kuimarika kwa kasi kubwa zaidi katika miaka ijayo.