Mwanamke Afrika Kusini afungwa maisha jela kwa kumuuza binti yake
(last modified Fri, 30 May 2025 07:32:32 GMT )
May 30, 2025 07:32 UTC
  • Mwanamke Afrika Kusini afungwa maisha jela kwa kumuuza binti yake

Mwanamke mmoja kutoka Afrika Kusini amehukumiwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kumuza binti yake mwenye umri wa miaka sita. Kwa mujibu wa nyaraka za mahakama, mtoto huyo aliyetambulika kwa jina la Joshlin Smith, aliuzwa kwa kiasi cha takribani dola 1,122 za Marekani (sawa na R20,000).

Ingawa watu watatu waliopatikana na hatia ya utekaji na biashara haramu ya Joshlin Smith walihukumiwa kifungo cha maisha siku ya Alhamisi, Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa juhudi za kumtafuta mtoto huyo bado zinaendelea.

Joshlin hajapatikana tangu alipotoweka kutoka nyumbani kwao eneo la Middelpos, Saldanha Bay mnamo 19 Februari 2024. 

Mama yake mzazi, Racquel ‘Kelly’ Smith, mchumba wake Jacquen ‘Boeta’ Appollis, pamoja na mtu wa karibu wa familia yao, Steveno ‘Steffie’ van Rhyn, walipatikana na hatia mapema mwezi huu katika Mahakama Kuu ya Western Cape.

Alhamisi hii, mahakama iliwahukumu kifungo cha maisha kwa kosa la biashara ya binadamu, na miaka 10 ya ziada kwa kosa la utekaji nyara.

Watatu hao wameonesha nia ya kukata rufaa, japokuwa hawakutoa ushahidi wowote kwa utetezi wao wakati wa kesi.

Katika taarifa rasmi, Kamishna wa Polisi wa Mkoa wa Western Cape, Luteni Jenerali Thembisile Patekile, aliwapongeza maafisa wote, wapelelezi, na wataalamu waliohusika katika kesi hiyo. Alisema:

“Uadilifu wenu unaakisi kilele cha utumishi wa vyombo vyetu vya usalama na umeleta tumaini kwa familia zinazongoja haki zipatikane.”

Taarifa hiyo ilisisitiza kuwa msako wa kumtafuta Joshlin haujasitishwa.

Natasha Andrews, mama wa ubatizo wa Joshlin, alisema kimya cha watuhumiwa hao wakati wa kusomwa kwa hukumu kimezidi kuumiza familia.

Kesi hiyo imewagusa watu wengi nchini humo, ambapo picha za mtoto Joshlin zimeenea kwenye mitandao ya kijamii, zikisindikizwa na ahadi ya zawadi ya randi milioni moja kwa yeyote atakayesaidia kumrejesha akiwa salama.