Namna mfumo wa Ubepari unavyowatumia wanawake kama nyenzo tu
Mfumo wa Ubepari umekuwa siku zote ukiwatumia wanawake kama nyenzo tu za kuuwezesha kupata faida zaidi.
Mfumo wa Ubepari, ambao ni moja ya miundo muhimu zaidi ya kiuchumi na kijamii ya dunia ya sasa, siku zote umekuwa ukijali kujiongezea faida na kujilimbikizia mitaji mikubwa zaidi. Katika kufikia lengo hilo, wanawake wamekuwa wakitumiwa kwa wingi kama nyenzo tu; kiasi kwamba, badala ya nafasi na mchango wao kupimwa kwa msingi wa haki za kiutu na hadhi sawa ya kijamii, unazingatiwa kulingana na ufanyaji kazi wao unaoweza kuwaletea faida kubwa zaidi mabepari. Uchunguzi wa suala hili unaonyesha kuwa, Ubepari umewatumia wanawake katika nyuga mbalimbali, kuanzia kwenye nguvukazi ya bei rahisi mpake kwenye matangazo ya kushajiisha uraibu wa matumizi, pamoja na propaganda na uenezi ili kuimarisha ukiritimba wake na kujiongezea faida na pato lake.
Miongoni mwa maeneo ya kwanza ya kutumiwa wanawake kama nyenzo katika mfumo wa Ubepari ni kwenye soko la ajira. Katika jamii nyingi za kibepari, wanawake hutumiwa kama nguvukazi ya bei rahisi zaidi kulinganisha na wanaume. Jambo hilo, sio tu linapunguza gharama za uzalishaji kwa waajiri, lakini pia linawezesha kuwatumikisha na kuwanyonya zaidi vibarua wa kazi. Katika sekta nyingi, hususan za ushoni wa nguo, utoaji huduma, na kazi za majumbani, wanawake hufanyishwa kazi kwa mishahara ya chini zaidi; na hufanya kazi hizo katika mazingira magumu zaidi kulinganisha na wanaume. Kwa kuweka pengo hilo la mishahara kati ya wanawake na wanaume, Ubepari hulitumia suala hilo kama wenzo wa kujiongezea faida.
Mbali na soko la ajira, mfumo wa Ubepari hutumia pia wanawake kama nyenzo za matangazo ya propaganda na kuvutia masoko ya bidhaa zake. Taswira ya mwanamke katika tangazo la biashara huwa mara nyingi inaonyeshwa kwa njia iliyozoeleka ya kuchochea ngono ili kuzidisha mvuto wa bidhaa na huduma zinazotangazwa. Aina hii ya utumiaji wa kinyenzo, sio tu hupelekea kudunishwa hadhi ya wanawake, lakini pia huwageuza kuwa chombo cha kuchochea uraibu wa manunuzi. Kwa kutumia miili na picha za wanawake, Ubepari huchochea hamu ya ununuzi na matumizi katika jamii na kujipatia faida zaidi. Katika muundo huo, wanawake huwa kwa kweli hawaonekani kama wanadamu huru, bali huwa kama wenzo tu wa kuuzia bidhaa na huduma.
Kwa upande mwingine, Ubepari unaeneza utamaduni wa ununuzi na matumizi na kuwafanya wanawake kuwa moja ya makundi walengwa yenye umuhimu katika soko la bidhaa. Bidhaa na huduma nyingi, hasahasa katika uga wa staili, urembo na mtindo wa maisha, zimebuniwa na kutangazwa ili kuwalenga zaidi wanawake, jambo ambalo huwaweka wao kwenye mashinikizo ya kijamii na kiutamaduni ya kushawishika kila mara kununua na kutumia bidhaa mpya. Ubepari huyatumia mashinikizo hayo ili kudumisha mzunguko wa matumizi na kujiongezea faida. Na kwa upande wa wanawake, wao huwa hawabaki kuwa wanunuzi wa kawaida tu, bali hugeuzwa kuwa wateja maalumu wa kudumu wanaohitaji kila mara kubuniwa bidhaa na huduma zingine mpya.
Yote haya tuliyoeleza yanaonyesha kuwa, Ubepari sio tu haujali suala la usawa wa kijinsia, lakini pia unalitumia pengo hilo kama njia ya kujiongezea faida. Hali hii inazidi kuweka wazi haja ya kuifanyia ukosoaji na upinzani mkubwa miundo ya Ubepari; kwa sababu ni kwa kuleta mabadiliko ya kimsingi katika mfumo huo, ndipo itawezekana kurejesha hadhi ya kweli na ya kiutu ya wanawake.
Kwa kumalizia inapasa tuseme kwamba, katika mfumo wa Ubepari, wanawake hutumika kama nyenzo tu za kujipatia faida zaidi badala ya kutambuliwa kama wanadamu huru na wenye haki sawa za kiutu. Mtazamo kama huu, sio tu unaendeleza pengo la kukosekana usawa wa kijinsia, lakini pia linaitia doa heshima ya kiutu ya wanawake. Kwa muktadha huo, kuufanyia ukosoaji na kukabiliana nao utumiaji huo wa kinyenzo, ni sehemu isiyotenganika ya mapambano ya kutetea haki na uadilifu wa kijamii na ya kulinda heshima na shakhsia halisi ya mwanamke…/