Nchi za Afrika zaanzisha mpango wa kuwalinda Albino
Kongamano la siku tatu la kikanda kuhusu ulemavu wa ngozi barani Afrika limehitimishwa nchini Tanzania ambapo mpango wa kwanza kabisa wa utekelezaji umeanzishwa.
Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia 17-19 Juni uliandaliwa na Mtaalam Huru wa Umoja wa Mataifa, Ikponwosa Ero na washirika wake na kuhudhuriwa na washiriki 150 kutoka nchi 29 za kanda ya Afrika ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za kitaifa za haki za binadamu, wanaharakati, wataalam wa haki za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika pamoja na wasomi.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, nchini Tanzania Bw. Alvaro Rodriguez amesema, 'usawa, utu na haki ndizo nguzo zinazopaswa kutuongoza katika mahusiano yetu na watu wenye ulemavu wa ngozi'.
Mpango wa utekelezaji wa Mkutano huu wa kwanza katika Bara la Afrika unao uwezo wa kufanya kuwa historia na kusahaulika mateso na ukosefu wa usawa ambao watu wenye ulemavu wa ngozi hukumbana nao.
Washiriki wa kongamano hilo waliitikia wito wa kutekeleza hatua za kuzuia, kulinda, uwajibikaji na kupambana na ubaguzi dhidi ya Albino.
Aidha waliahidi kutekeleza baadhi ya hatua hizo maalum kwa kufanya kazi na kulishughulikia suala hilo kitaifa, kutenga bajeti kwa ajili ya suala hilo na kuweka mtu au kamati ya kukabiliana na mgogoro huo katika kila eneo.
Mpango wa utekelezaji ulioandaliwa utatahtminiwa na Mtaalam wa Umoja wa Mataifa kwa mwaka mmoja ujao na utakuwa kama kiwango cha bara zima cha kuwafanya wadau wote, hasa serikali, kuwajibika.