AU yasisitiza ulazima wa kusitishwa mapigano haraka huko Sudan
Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amesiistiza ulazima wa kusimamishwa vita haraka iwezekanavyo kati ya pande zinazopigana nchini Sudan.
Musa Faki Mahamat amesisitiza katika mkutano wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya intaneti kwamba kuna haja ya kusimamishwa mapigano mara moja huko Sudan. Amesema kuwa shughuli za kibinadamu, usambazaji misaada kwa raia na kukabidhiwa madaraka kwa raia nchini Sudan vinapaswa kupewa mwanya. Amesema njia za kijeshi si suluhisho kwa mgogoro wa nchi hiyo.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika pia limetoa taarifa likieleza kuwa mgogoro wa Sudan hauna ufumbuzi wa kijeshi na kwamba vita na mapigano vinapasa kusimamishwa haraka iwezekanavyo bila ya masharti yoyote. Taarifa ya AU imeongeze kuwa, hadi kufikia tarehe 9 Mei mwaka huu watu zaidi ya 700,000 walikimbia mapigano huko Sudan na kuwa wakimbizi katika nchi jirani.
Mapigano ya silaha yalianza Sudan Aprili 15 mwaka huu kati ya vikosi vya jeshi la serikali linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) vinavyoongozwa na Muhammad Hamdan Dagalo. Ripoti za mashirika ya kimataifa zinaeleza kuwa watu karibu milioni 25 wa Sudan, yaani nusu ya jamii nzima ya nchi hiyo, wanahitaji misaada ya kibinadamu.