Watoto 300 waliokwama waokolewa kutoka katika kituo cha mayatima huko Sudan
(last modified Fri, 09 Jun 2023 06:46:03 GMT )
Jun 09, 2023 06:46 UTC
  • Watoto 300 waliokwama waokolewa kutoka katika kituo cha mayatima huko Sudan

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa Unicef limeeleza kuwa, watoto wasiopungua 300 wa rika mbalimbali wakiwemo wachanga wameokolewa kutoka katika kituo cha kulelea mayatima huko Khartoum mji mkuu wa Sudan baada ya kutelekezwa huko huku mapigano yakiendelea nchini humo.

Watoto hao wameondolewa katika kituo hicho cha kulea mayatima huko Khartoum baada ya watoto 71 kuaga dunia kwa njaa na magonjwa mbalimbali kituoni hapo tangu katikati ya Aprili mwaka huu. Mkasa huo katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Mayqoma uligonga vichwa vya habari mwishoni mwa mwezi uliopita wakati mapigano yakiendelea kati ya vikosi vya jeshi la Sudan na vile vya  Msaada wa Haraka (RSF).

Mapigano Sudan kati ya jeshi na vikosi vya RSF

Ricardo Pires Msemaji wa Shirika la Unicef ameeleza kuwa watoto hao wasiopungua 300 katika kituo cha kulea watoto yatima cha Al- Mayqoma huko Khartoum wamehamishwa katika sehemu yenye usalama huko kaskazini mashariki mwa Sudan. Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Afya za Sudan ndio zimechukua jukumu la kuwasimamia watoto hao huku Unicef ikitoa misaada ya kibinadamu ikiwa ni pamoja na dawa za matibabu, chakula, na vifaa vya elimu na michezo. Watoto hao wana umri kuanzia mwezi mmoja hadi miaka 15.

Msemaji wa Unicef ameongeza kuwa, watoto hao wasiopungua 300 tayari wamefanyiwa uchunguzi wa kidaktari kufuatia safari yao ndefu kuelekea katika makazi mapya na kwamba mtoto yoyote atakayehitaji kulazwa hospitali atafikishwa mara moja. Watoto hao sasa wamepatiwa makazi huko Madani makao makuu ya jimbo la Jazira umbali wa kilomita 135 kusini mashariki mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

 

Tags