Johnson & Johnson yashtakiwa Kenya kwa kuwauzia watu poda iliyopigwa marufuku Ulaya, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i98734-johnson_johnson_yashtakiwa_kenya_kwa_kuwauzia_watu_poda_iliyopigwa_marufuku_ulaya_marekani
Shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini Kenya limeshtaki shirika la kimataifa la Marekani, Johnson & Johnson, kwa kosa la kuwauzia Wakenya poda ya ulanga.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 13, 2023 08:46 UTC
  • Johnson & Johnson yashtakiwa Kenya kwa kuwauzia watu poda iliyopigwa marufuku Ulaya, Marekani

Shirika moja la kutetea haki za binadamu nchini Kenya limeshtaki shirika la kimataifa la Marekani, Johnson & Johnson, kwa kosa la kuwauzia Wakenya poda ya ulanga.

Shirika la African Centre for Corrective and Preventive Action limesema kuwa ingawa bidhaa hiyo ilipigwa marufuku katika nchini kama vile za Bara Ulaya na India bado inauzwa nchini Kenya.

Katika ombi lililowasilishwa lenye kuangazia kulinda haki ya mnunuzi, shirika hilo linadai kuwa kampuni ya Johnson & Johnson linatumia benzene na talc kwenye bidhaa zake za poda ya watoto.

Shirika hilo linadai kuwa benzene na talc inasababisha saratani kwa binadamu na kuwa ‘’ talc yenye madini ya asbesto husababisha madhara makubwa kwa mtumiaji wake.’’

Mapema mwezi Aprili mwaka huuuu pia Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilitangaza kuwa linachunguza uwezekano wa kuwepo kwenye soko poda za watoto zinazotengenezwa na kampuni kubwa ya dawa ya Marekani, Johnson & Johnson (J&J), ambazo imebainika kuwa zinasababisha saratani.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Athuman Ngenya amesema shirika hilo limeanza kukusanya sampuli za poda za J&J kwa ajili ya uchunguzi mpya wa kimaabara.

Hatua hiyo ya TBS ilichukuliwa baada ya J&J kupendekeza kutoa Dola za Kimarekani bilioni 8.9 ili kutatua kesi za miaka mingi zinazodai kuwa bidhaa zake za poda zimesababisha maradhi ya saratani.

Uchunguzi: Poda za Johnson Johnson zinasababisha saratani

Kundi la mawakili ambao wanawakilisha karibu walalamikaji 70,000 nchini Marekani, ikiwa ni pamoja na familia za watu waliokufa kutokana na saratani ya ovari na mesothelioma, wameelezea mpango huo kama ushindi mkubwa kwa makumi ya maelfu ya wanawake wanaosumbuliwa na saratani ya uzazi inayosababishwa na bidhaa za J.&J.

Mnamo 2020, kampuni hiyo ilisema itasitisha uuzaji wa poda yake ya watoto zenye mada ya talc nchini Marekani na Canada. Kampuni hiyo imesema inapanga kuacha kuuza bidhaa hiyo duniani kote mwaka huu.