Mapigano juu ya mageuzi ya katiba yaua watu 9 Puntland, Somalia
Watu wasiopungua tisa wameuawa katika mapigano yaliyosababishwa na suala tata la kuifanyia marekebisho katiba katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.
Dakta Abdrisak Ahmed, afisa wa afya katika Hospitali ya Umma ya Garowe amesema hospitali hiyo imepokea maiti tisa na majeruhi 12 wa mapigano hayo yaliyoripuka jana Jumanne katika mji wa Garowe, makao makuu ya eneo la Puntland.
Wafuasi wa upinzani wanamtuhumu kiongozi wa eneo hilo, Said Abdullahi Deni, kwamba anataka kuifanyia marekebisho katiba kwa shabaha ya kurefuisha kipindi chake cha uongozi kinachopasa kumalizika Januari mwaka ujao.
Mjadala umepamba moto hivi sasa katika Bunge la Puntland kuhusu uwezekano wa kurekebisha katika na kubadilisha mfumo wa uchaguzi katika eneo hilo lililoko kaskazini mashariki mwa Somalia.
Bunge hilo la eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland lilimchagua Said Abdullahi Deni kuwa rais eneo hilo mnamo Januari mwaka 2019, kuchukua nafasi ya Abdiweli Mohamed Ali Gaas.
Mbali na hujuma za al-Shabaab na makabiliano ya wenyewe kwa wenyewe, eneo hilo limekuwa likishuhudia mapigano baina yake na maeneo jirani. Mwaka 2016, askari wa eneo la Puntland na GalMudug walipambana kwa wiki kadhaa kugombania udhibiti wa eneo lenye utata la Galkayo.
Aidha vikosi vya maeneo yenye mamlaka ya ndani ya Somaliland na Puntland nchini Somalia vilishambuliana na makumi ya watu kuuawa, katika vita vya kung'ang'ania wilaya ya Tuqarak, katika eneo la Sool.