Wanamgambo washambulia gereza katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131606-wanamgambo_washambulia_gereza_katika_mji_mkuu_wa_somalia_mogadishu
Sauti za milipuko na risasi zilisikika pakubwa jana huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia baada ya wanamgambo kushambulia gereza karibu na ikulu ya rais.
(last modified 2025-10-05T07:36:07+00:00 )
Oct 05, 2025 07:36 UTC
  • Wanamgambo washambulia gereza katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Sauti za milipuko na risasi zilisikika pakubwa jana huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia baada ya wanamgambo kushambulia gereza karibu na ikulu ya rais.

Moshi ulionekana ukitoka upande wa juu wa gereza la Godka Jilacow ambalo pia linatumika kama makao makuu ya kitengo cha intelijinsia cha jimbo. 

Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba wanamgambo hao walitumia gari linalofanana na lile linalotumiwa na vikosi vya usalama vya kitengo hicho, na kwamba askari jeshi walifanikiwa kuzima shambulio hilo na kuwaua wanamgambo kadhaa.

Shambulio dhidi ya gereza huko Mogadishu lilitekelezwa jana masaa kadhaa baada ya serikali kuondoa vizuizi vya barabarani vilivyokuwa vimedumu huko Mogadishu kwa miaka kadhaa kufuatia kuboreka hali ya usalama. 

Vizuizi hivi viliwekwa ili kulinda maeneo muhimu ya serikali, hata hivyo wakaazi wengi wa mji mkuu Mogadishu walikuwa wakialamika kwamba vilikuwa vikisababisha trafiki na kutatiza biashara.

Kundi la wanamgambo wa al Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida lenye makao yake nchini Somalia limedai kuhusika na shambulio katika gereza huko Mogadishu. Limesema kuwa limefanikiwa kuwaachia huru baadhi ya wafungwa.