Miripuko pacha yatikisa Somalia, kadhaa wapoteza maisha
Watu kadhaa wanahofiwa kuuawa katika mashambulizi pacha ya mabomu katika mji wa Bardhere ulioko katika eneo la Gedo, kusini magharibi mwa Somalia.
Kwa mujibu wa Adan Aw Hirsi, Waziri wa Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa Somalia, hujuma hizo zimelenga kambi ya wanajeshi wa Somalia pamoja na askari wa Ethiopia wanaohudumu chini ya mwavuli wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS).
Ingawaje hakuna kundi lililotangaza kuhusika na mashambulizi hayo hadi tunaenda mitamboni, lakini waziri huyo amesisitiza kuwa, "Al-Shabaab na wafadhili wao kamwe hawatatutisha na hujuma za namna hii."
Wakazi wa Bardhere wameliambia shirika la habari la Anadolu kuwa, makabiliano makali ya risasi yalijiri baada ya kutokea mashambulizi hayo pacha.
Shambulizi hilo limejiri katika hali ambayo, Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS) kimetangaza kuwa, kimekabidhi kambi ya kijeshi ya jimbo la Hirshabelle kwa vikosi vya Somalia na hivyo kuanza mchakato wa kuondoa nchini humo askari wake 2000.
Vikosi vya ATMIS ambavyo vinajumuisha takriban wanajeshi elfu 20, polisi na raia kutoka nchi za Uganda, Burundi, Djibouti, Ethiopia na Kenya, Aprili 2022 vilichukua nafasi ya vikosi vya AMISOM vilivyotumwa nchini Somalia tangu mwaka 2007 kupambana na uasi wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab.